Kushindwa katika uchaguzi ni jambo la kawaida - Moses Kuria

Muhtasari

• Moses Kuria amewataka viongozi wanaopoteza uchaguzi kukubali matokeo na kusonga mbele na maisha yao.

• Alisema kwamba kuna nafasi chache za uongozi hivyo sio kila mtu anayewania ataingia mamlakani.

Mbunge wa Gatundu kusini Moses Kuria amesema kwamba kutofanikiwa kushinda katika uchaguzi ni jambo la kawaida ambalo halipaswi kumkosesha mwanasiasa yeyote usingizi.

Kupitia ujumbe aliochapisha katika ukurasa wake wa Facebook, Kuria alisema kwamba idadi ya nafasi za uongozi ni chache mno kwa hiyo sio kila anayegombea ataingia mamlakani.

Kuria alisema kwamba kutoshinda uchaguzi hakupaswi kuzua hali ya vurugu katika taifa, kwani kuna mambo mengi wanayoweza kuyafanya na kuendeleza maisha yao hata baada ya uchaguzi.

''Kutoshinda cheo sio swala la kutisha, halipaswi kuyumbisha amani ya taifa," Kuria alisema.

Kulingana naye, ni viongozi 1,882 tu kati ya wakenya 50M  ambao wanaweza kuingia mamlakani,  na kuwasihi wagombea wanaoshindwa kujishughulisha na kazi tofauti kama wakenya wengine.

Kauli ya Kuria inajiri wakati joto la kisiasa linazidi kupanda nchini, huku wanasiasa mbalimbali wakipambana usiku na mchana kuingia mamlakani.

Wakichapisha maoni yao kwenye 'comment section' wafuasi wake walimtaja Kuria kuwa kiongozi mwenye maono na ukomavu mkubwa katika siasa kutoka na kauli hiyo.

Katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, Kuria atakuwa anagombea wadhfa wa ugavana katika kaunti ya Kiambu kupitia tikiti ya Chama cha Kazi kilichopo chini ya muungano wa kenya Kwanza.