Mguu niponye!Ruth Odinga alazimika kukimbilia usalama baada ya machafuko kuzuka Kisumu

Muhtasari
  • Ruth Odinga alazimika kukimbilia usalama baada ya machafuko kuzuka
KInara wa ODM Raila Odinga
Image: George Owiti

Machafuko yalizuka katika kituo cha kupigia kura cha Urudi huko Nyakach, kaunti ya Kisumu wakati wa uteuzi wa chama cha ODM na kuwalazimu polisi kufyatua risasi hewani ili kutawanya umati wa watu waliokuwa na ghasia.

Tukio hilo lilisitisha kwa muda zoezi la upigaji kura ambalo baadaye lilianza tena baada ya utulivu kurejea.

Aliyekuwa Naibu Gavana wa Kisumu, Ruth Odinga alikuwa akiondoka katika kituo cha kupigia kura wakati machafuko yalipoanza kulazimisha usalama wake kumtorosha.

Alikuwa amepokea wasiwasi kutoka kwa wapiga kura kwamba kulikuwa na mtu anayedaiwa kuendesha zoezi la upigaji kura sambamba.

Asubuhi alipotembelea vituo mbalimbali vya kupigia kura, Ruth alitoa wito kuwe na mchujo wa chama wenye amani, huru, wa haki na unaoaminika.

Madai hayo yalizua shaka miongoni mwa wapiga kura waliodai kura za mchujo huru, za haki na za kuaminika.

OCPD wa Nyakach Daniel Chacha alithibitisha kuwa kulikuwa na makabiliano kati ya mwaniaji aliyevamia kituo cha kupigia kura cha Urudi na maafisa wa ODM. Mwaniaji huyo ambaye Chacha hakumtaja alirushiana maneno na maafisa wa chama lakini suala hilo likazuiwa.

Alisema atatoa maelezo zaidi baadaye.