"Nitaliangazia hilo nikiingia ofisini Agosti 9" Ngirici adai Waiguru alimuomba msamaha, akakataa

Muhtasari

• Mwakilishi wa kike wa Kirinyaga Purity Wangui Ngirici alidai kwamba alikutana na Waiguru ambaye alimuomba samahani lakini akapuuzilia na kusema ataliangalia akiingia ofisini.

Mwakilishi wa kike katika kaunti ya Kirinyaga Wangui Ngirici amezua maswali mengi kuliko majibu kwenye ukurasa wake wa Facebook baada ya kudai kwamba Jumatatu alikutana uso kwa uso na mpinzani wake mkuu ambaye alimuomba samahani lakini akaipuuza na kusema atakuja kuitathmini pindi atakapoingia ofisini baada ya uchaguzi wa Agosti 9.

Ngirici ambaye anawania ugavana wa kaunti ya Kirinyaga kama mgombea huru baada ya kuondoka kambi ya naibu rais William Ruto alibainisha wazi kwamba mpinzani wake huyo ni mwanamke ambapo hili lilifungua fikira za wengi na kujua wazi kwamba alikuwa anazungumzia gavana wa sasa Ann Waiguru ambaye pia anawania kukitetea kiti hicho kwa tiketi ya chama cha UDA.

“Nilikutana na mmoja wa wapinzani wangu mapema leo na (mwanamke) huyo alisema kwa upole ‘samahani’. Nitaliangazia hilo pindi nitakapoingia ofisini Agosti 9 mwaka 2022,” aliandika Ngirici.

Baada ya kuona maswali yamezidi kuliko majibu katika upande wa kutoa maoni kwenye post hiyo, Ngirici alilemaza kipengele hicho na kuzuia watu kutoa maoni zaidi.

Mwaka jana, Ngirici alikigura chama cha UDA kwa kuteta kwamba chama hicho kilikuwa na njama ya kumdhulumu kwa kumpatia Waiguru tiketi ya moja kwa moja ambapo alijiunga na Jubilee lakini hivi majuzi akapakia post fulani ya kudokeza kwamba amekihama chama hicho na sasa atawania kama mgombea huru.