Azimio watangaza mikakati yao ya kushinda uchaguzi na kuchagua mgombea mwenza wa Odinga

Muhtasari

• Muungano wa Azimio la Umoja - One Kenya Alliance umetoa maelezo kuhusu mazungumzo yao na wanachama wa vuguvugu hilo.

• Walisema wanalenga kuhakikisha wanashinda uchaguzi wa Agosti 9.

Viongozi wa muungano wa Azimio la Umoja - One Kenya Alliance
Viongozi wa muungano wa Azimio la Umoja - One Kenya Alliance
Image: Fredrick Omondi

Vuguvugu la Azimio la Umoja- One Kenya Alliance likiongozwa na rais Uhuru Kenyatta leo Alhamisi katika jumba la KICC limeweka wazi maelezo ya mazungumzo yao kuhusu mikakati waliyo nayo  kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9,kusuluhisha tofauti zilizopo  na kuhakikisha wanaibuka kidedea katika kinyang'anyiro hicho.

Wakitoa taarifa yao kupitia kwa mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohammed, walisema kwamba wataunda bodi kuu ya muungano wa kitaifa ambayo itakuwa na bodi mbalimbali zikiwemo:

• Bodi ya uchaguzi katika muungano

• Kamati ya kitaifa ya nidhamu

• Bodi ya rufaa katika muungano

• Bodi ya kutatua migogoro katika muungano

Bodi hizo zitahakikisha kwamba zinabuni mbinu na mikakati faafu ya kampeni  kuhakikisha muungano wa Azimio la Umoja - One Kenya Alliance unaunda serikali ijayo.

Vilevile zitahakikisha kwamba vuguvugu hilo linashinda nyadhfa nyingi katika serikali za kaunti na katika bunge la kitaifa.

Walijukimishwa kuhakikisha kwamba kunakuwa na mazingira mazuri ya ukuzi wa uchumi na umoja katika taifa hata baada ya uchaguzi mkuu.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga alifika eneo la mkutano mwendo wa saa mbili asubuhi. Baadaye alimkaribisha Rais Uhuru ambaye aliwasili mwendo wa saa 8.30 asubuhi.

Viongozi wengine ambao wanahudhuria mkutano huo ni Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, Gavana wa Mombasa Hassan Joho, kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua, mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi, Kinara wa DAP Mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi, Mbunge wa Taveta Naomi Shaban na Gavana wa Kitui Charity Ngilu.

Aidha ,walipendekeza kubuniwa kwa jopo la ushauri ambalo litatambua watu faafu ambao wanaweza kuchukua nafasi ya mgombea mwenza wa Raila Odinga.

Ikumbukwe kwamba suala la mgombea mwenza wa Azimio-One Kenya Alliance limetishia kusambaratisha muungano huo na ni moja wapo wa hoja zinazojadiliwa.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka amekuwa akishikilia kuwa yeye ndiye bora zaidi kwa nafasi hiyo, huku baadhi ya viongozi wa kike kutoka muungano wa Azimio wakitaka Martha Karua atajwe mgombea mwenza wa Raila.

Rais Uhuru Kenyatta ndiye mwenyekiti wa baraza kuu la chama cha muungano wa Azimio- One Kenya huku Raila akiwa kiongozi wa chama na mpeperushaji bendera ya urais.

Mbali na rais Kenyatta na Raila Odinga, viongozi Wanachama wa baraza hilo ni Kinara wa Wiper Kalonzo, Martha Karua wa Narc Kenya, Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi, Charity Ngilu wa Narc, Wafula Wamunyinyi wa DAP-K, Mwakilishi wa Wanawake wa Muranga Sabina Chege, Abdi Noor Omar Farah na Mbunge wa Taveta Naomi Shaban.