"Sijui nilie ama niombe" Bahati azungumza baada ya kutwaa tikiti ya Jubilee Mathare

Muhtasari

• Kanini Kega alimkabidhi Bahati cheti cha uteuzi  siku ya Ijumaa katika makao makuu ya chama hicho.

•Bahati aliwashukuru vinara wakuu wa muungano wa Azimio la Umoja, rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga kwa kuwa na imani naye.

Image: INSTAGRAM// BAHATI

Ni rasmi kwamba mwanamuziki Kelvin Kioko almaarufu Bahati ndiye atakayepeperusha bendera ya Jubilee katika kinyang'anyiro cha ubunge wa eneo la Mathare.

Mkurugenzi wa uchaguzi  wa Jubilee, Kanini Kega alimkabidhi Bahati cheti cha uteuzi  siku ya Ijumaa katika makao makuu ya chama hicho.

Bahati ambaye alijitosa kwenye ulingo wa siasa mwezi uliopita ametaja uteuzi huo kama ndoto iliyoafikia sio kwake binafsi tu bali pia kwa vijana na wakazi wa Mathare.

"Sijui jinsi ya kusherehekea haya. Sijui nilie au niombe. Hii ni ndoto iliyotimia, sio kwangu tu kama Bahati; bali pia kwa vijana na watu wangu wa Mathare ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiombea mbunge aliyetengenezewa Mathare," Bahati alisema kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Mwanamuziki huyo alikabidhiwa tikiti ya chama hicho tawala baada ya kuchaguliwa kama mgombea kiti maarufu zaidi katika eneo bunge la Mathare.

Aliwashukuru vinara wakuu wa muungano wa Azimio la Umoja, rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga kwa kuwa na imani naye.

" Ni mwamko mpya kwa watu wangu. Ni wakati wa Mathare mpya. Utukufu uwe kwa Mungu milele," Alisema.

Mamia ya wanamitandao wakiwemo watu mashuhuri  wameendelea kutuma pongezi kwa mwanamuziki huyo.

Bahati anatazamia kumridhi Tom Oluoch ambaye amekalia kiti hicho kwa sasa.