Mgombea mwenza: Raila aunda jopo kusaka mgombea mwenza

Muhtasari

• Wanachama wa jopo hilo ni Bishop Peter Njenga, archbishop Zacheous Okoth, Seneta Enoch Wambua, Michael Orwa,  Noah Wekesa, Sheikh Mohammed Khalifa, na Beatrice Meo.

Raila Odinga
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Mgombeaji wa urais wa muungano wa Azimio – One Kenya, Raila Odinga ameunda jopo la watu saba kusaka mgombea mwenza wake.

Wanachama wa jopo hilo ni Bishop Peter Njenga, archbishop Zacheous Okoth, Seneta Enoch Wambua, Michael Orwa,  Noah Wekesa, Sheikh Mohammed Khalifa, na Beatrice Meo.

Jopo hilo litaongozwa na Beatrice Meo kama mwenyekiti wake.

Akitangaza majina ya wanachama wa jopo hilo, katibu wa baraza la muungano wa Azimio – One Kenya, Junet Mohamed alisema kwamba Raila aliteua jopo hilo baada ya kushauriana na baraza kuu la muungano huo.

Kulingana na Junet yule ambaye atateuliwa kama mgombea mwenza lazima awe anaafikia vigezo muhimu vya katiba kama vile uadilifu, heshima kwa wananchi na awe mtu aliyejitolea kutumikia taifa.

Jopo hilo linafaa kuwapiga msasa wanaotaka kuchukuwa nafasi ya mgombea mwenza wa Raila na kisha kuwasilisha jina au majina ya waliofuzu kwa baraza kuu la muungano huo tarehe 10 mwezi Mei au kabla ya tarehe hiyo.

Suala la mgombea mwenza limekuwa msumari moto katika muungano wa Azimio – One Kenya na katika mungano wa naibu rais William Ruto Kenya Kwanza huku kila mtu akivuta upande wake.