Raila aahidi kukabiliana na ufisadi na kupunguza deni la kitaifa

Muhtasari

• Akizungumza katika ziara yake nchini Marekani Kinara wa muungano wa Azimio – One Kenya, Raila Odinga  alisema juhudi zake zitaangazia pia kupunguza deni la kitaifa.

• Raila alisema serikali ya Azimio imeratibu vita dhidi ya ufisadi, uboreshwaji miundo msingi, sekta za afya na elimu kama baadhi ya agenda zake kuu punde tu itakapochaguliwa mamlakani .

Kinara wa Azimio - One Kenya Raila Odinga akizungumza katika ziara yake nchini Marekani.
Kinara wa Azimio - One Kenya Raila Odinga akizungumza katika ziara yake nchini Marekani.
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Serikali ya Muungano wa Azimio – One Kenya chini ya uongozi wa Raila Odinga utavipa vita dhidi ya ufisadi kipau mbele.

Akizungumza katika ziara yake nchini Marekani siku ya Jumanne, Kinara wa muungano wa Azimio – One Kenya, Raila Odinga pia alisema juhudi zake zitaangazia sana kupunguza deni la kitaifa.

Raila alisema kwamba serikali ya Azimio imeratibu vita dhidi ya ufisadi, uboreshwaji miundo msingi, sekta za afya na elimu pamoja na kuwawezesha kina mama kama baadhi ya agenda zake kuu punde tu itakapochaguliwa mamlakani Agosti 9  mwaka huu.

Wajumbe waliofika kusikiza hotuba ya kiongozi wa Azimio - One Kenya
Wajumbe waliofika kusikiza hotuba ya kiongozi wa Azimio - One Kenya
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Kiongozi wa Azimio aliahidi kuboresha zaidi uhusiano kati ya Kenya na mataifa ya nje kwa lengo la kukuza uchumi wa taifa.

Raila alikuwa akizungumza mjini Washington DC alipokutana na kongamano la Africa group lenye makao yake nchini Marekani.

 Odinga amekariri kuweka mikakati dhabiti ili kukabiliana na changamoto zinazozidi kulikumba taifa la Kenya miaka 50 baada ya kupata uhuru.

Aliyekuwa balozi wa Marekani nchini Kenya Johnnie Carson (Kushoto) akiwa miongoni mwa watu mashuhuri waliojitokeza kusikiza hotuba ya Raila.
Aliyekuwa balozi wa Marekani nchini Kenya Johnnie Carson (Kushoto) akiwa miongoni mwa watu mashuhuri waliojitokeza kusikiza hotuba ya Raila.

Raila aliwarai wawekezaji kuzuru Kenya na kuwekeza kwa sababu utawala wake utaweka mazingira bora kwa kila muwekezaji kunawiri.

Kiongozi huyo na ujumbe wake wamelazimika kukatiza ziara ya Marekani ili kurejea nchini Kenya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa rais wa tatu Kenya Mwai Kibaki aliyefariki Ijumaa iliyopita.