Mwanasiasa wa UDA aomba msamaha baada ya kurekodiwa akiwatupia watu vipande vya keki 'kama kuku'

Muhtasari

•Muratha amekiri kuwa hakutumia njia mwafaka kusambaza keki ambayo alikuwa amepatiwa jukumu la kusimamia. 

•Mtaalamu huyo wa masuala ya ndoa ameweka wazi kuwa amejuta matendo yake na kuahidi kutorudia kosa hilo tena.

Image: FACEBOOK// ANNE MURATHA

Mgombea kiti cha mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kiambu kwa tikiti ya UDA Anne Muratha amekiri kuwa alitupa vipande vya  keki kwa umati wa watu uliokuwa umejumuika katika uwanja wa Ruiru.

Katika taarifa yake ya Jumatano, Muratha amesema video ambayo imekuwa ikisambazwa mitandaoni ilirekodiwa mnamo Novemba 7, 2021.

Mwanasiasa huyo hata hivyo amekiri kuwa hakutumia njia mwafaka kusambaza keki ambayo alikuwa amepatiwa jukumu la kusimamia. 

"Ningependa kuthibitisha kuwa mimi ndiye niliyenaswa katikavideo inayosambaa nikirusha vipande vya keki kwa umati wa watu waliokuwa wamekusanyika katika Uwanja wa Ruiru kwa hafla iliyofanyika Novemba 7, 2021. Nilikuwa msimamizi wa keki wa siku hiyo na nilishindwa kudhibiti umati na kusambaza keki ipasavyo," Muratha amesema kupitia Facebook.

Muratha ameomba msamaha kufuatia kitendo hicho chake ambacho kimeibua ghadhabu kubwa miongoni mwa wanamitandao.

"Ikiwa ningerudisha saa nyuma, ningesambaza keki tofauti. Mimi ni mama na mke ambaye ameazimia kupika keki kubwa zaidi ya nafasi kwa ajili ya wakazi wa Kiambu na kuwahudumia kwa bidii kama mwakilishi wao wa wanawake," Amesema.

Mtaalamu huyo wa masuala ya ndoa ameweka wazi kuwa amejuta matendo yake na kuahidi kutorudia kosa hilo tena.

Muratha alijipata  matatani baada ya video yake akitupia umati wa watu vipande vya keki kusambaa mitandaoni.

Katika video hiyo , Muratha alionekena akiwatupia watu vipande vya keki kama jinsi mfugaji anavyowatupia kuku wake mahindi. Watu waliokuwa wamejumuika pale wanaonekana wakiinua mikono yao juu katika juhudu za kufikia vipande vile vya keki.

Kabla ya kuanza kutupa keki ile, mtaalamu huyo wa masuala ya ndoa alisikika akiwaagiza wakazi wajipange vizuri ili kila mmoja aweze kufikiwa na kipande angalau.

Muratha alikosolewa sana kufuatia hayo huku wanamitandao wengi wakionekana kughadhabishwa na kitendo chake.