Ruto aambiwa kumchukuwa Kalonzo kama mgombea mwenza kama anamjali sana

Muhtasari

• Msemaji wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Alliance Makau Mutua amemthubutu Naibu Rais William Ruto kumchagua kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kama mgombea mwenza.

DP RUTO
Image: DOUGLAS OKIDDY

Msemaji wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Alliance Makau Mutua amemthubutu Naibu Rais William Ruto kumchagua kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kama mgombea mwenza.

Akijibu ujumbe wa naibu rais kuhusu kumdhalilisha Kalonzo, Mutua alisema unafiki wa Ruto ni hali ya juu na anafaa kumchagua kiongozi huyo wa Wiper ikiwa anamjali sana.

Alimkosoa Ruto kwa kujishughulisha na mambo yasiomhusu, akisisitiza kuwa maamuzi ya Azimio ni jumuishi, tofauti na yake.

"Ushauri wangu kwa @WilliamsRuto - tafadhali mchague @skmusyoka kama mgombea mwenza wako ikiwa unamjali sana. Unafiki wako ni wa juu. Tuachie mambo ya Azimio. Acha kunyoosha pua lako mahali pasipostahili. Maamuzi yetu ni jumuishi/shirikishi. Yako ni ya gizani," Mutua alisema.

Mutua alisema haya baada ya Ruto kulinganisha hatua ya kumhoji kiongozi wa Wiper kwenye mahojiano ya kusaka mgombea mwenza na kumdhalilisha.

Naibu rais a;isema kwamba kila kiongozi anastahili heshima.

Aliongeza kuwa ni lazima Wakenya waungane ili kuondoa tamaduni ya ukora katika siasa, jambo ambalo baadhi ya wanasiasa wanafahamika nalo.

"Ingawa sisi ni washindani, lakini kumuweka mheshimiwa Kalonzo kwenye 'mahojiano' ya kufedhehesha ni kumdhalilisha. Ni lazima tuungane kuondoa utamaduni wa ukora wa kisiasa, ambayo ni sifa ya baadhi ya wanasiasa. Kwa vyovyote vile kila kiongozi anastahili utu na heshima. Heshima si utumwa. ," aliandika kwenye twitter siku ya Jumatano.

Kiongozi mwenzake wa Kenya Kwanza Alliance, Moses Wetang'ula pia alisema kuwa Makamu huyo wa rais wa zamani anastahili heshima katika muungano wa Azimio na kwamba hasira kutoka kwa wafuasi wake ilikuwa ilifaa.

"Anafanya hivyo tena: kuwadharau na kuwadhalilisha wenzake. Sasa Mheshimiwa Kalonzo anajisujudu mbele ya wandani wa Raila ili kuonyesha "ubora wake kama mgombea mwenza. SKM unastahili bora zaidi! Hasira ya wandani wake inafaa," Wetang'ula alisema.

Mchakato wa uteuzi wa mgombea mwenza ulioundwa na Azimio umeibua uvumi kwamba huenda Kalonzo akapewa jukumu lingine tofauti.

Uvumi huu umezua taharuki katika kambi ya Kalonzo, huku washirika wake wakimtaka asiende kwenye mahojiano ya mgombea mwenza.

Wanahoji kuwa amekuwa makamu wa rais kwa miaka mitano, na kuwa mgombea mwenza wa Raila mara mbili. Wanasisitiza kuwa kwenda kwenye mahojiano itakuwa ni kumkosea heshima.

“Chaguo ni lake (Raila). Akitaka kuwa Rais amtafute Kalonzo. Sitamshauri kiongozi wa chama changu kufika mbele ya jopo lolote la uhakiki ili kuambiwa ataje majina yake kama yanavyoonekana kwenye kitambulisho. Huo ni upuzi,” Mbunge wa Makueni Daniel Maanzo alisema.