Jubilee yapendekeza Sabina Chege au Peter Kenneth kuwa mgombea mwenza wa Raila

Muhtasari

•Jubilee iliomba jopo la uteuzi wa mgombea mwenza wa Azimio kuzingatia Sabina Chege na Peter Kenneth.

•IEBC iliwapatia wagombea urais wote hadi Mei 16 kuwa wamefanya uamuzi wa wagombea wenza wao na kuwasilisha majina.

Mwakilishi wa Mwanamke wa Murang'a Sabina Chege, aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth na Mbunge wa Gatanga Joseph Nduati katika kanisa la Kiunyu PCEA.
Mwakilishi wa Mwanamke wa Murang'a Sabina Chege, aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth na Mbunge wa Gatanga Joseph Nduati katika kanisa la Kiunyu PCEA.
Image: MAKTABA

Chama tawala cha Jubilee kimewasilisha majina ya wanachama wake wawili ambao wanapendekeza kuwa wagombea wenza wa Raila.

Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, Jubilee iliomba jopo la uteuzi wa mgombea mwenza wa Azimio kuzingatia mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Murang'a Sabina Chege na mbunge wa zamani wa Gatanga Peter Kenneth. 

"Tunarejelea mada iliyo hapo juu na kutoa majina ya watu waliopendekezwa na Chama cha Jubilee ili kuzingatiwa kama Wagombea wenza wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya. Peter Kenneth na Sabina Chege," Taarifa iliyopigwa saini na mwenyekiti wa bodi ya Jubilee ya uchaguzi Stephen Wandeto ilisoma.

Haya yanajiri huku jopo la uteuzi wa mgombea mwenza wa Azimio ambalo linaongozwa na mbunge wa zamani Noah Wekesa likiendelea kuzingatia wanasiasa wanaopendekezwa kuchukua nafasi hiyo.

Vyama vyote 26 vya Azimio vinapaswa kuwasilisha majina ya wagombea wenza ambao vinapendekeza kabla ya jopo kukamilisha zoezi hilo mnamo Mei 10 na kuwasilisha jina la aliyependekezwa zaidi kwa Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga.

Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, Gavana wa Nakuru Lee Kinyajui na Waziri Peter Munya ni miongoni mwa wanasiasa wengine ambao wamependelewa kuchukua nafasi hiyo.

Siku ya Jumatano chama cha Kanu kinachoongozwa na seneta wa Baringo kilimpendekeza Kalonzo Musyoka kukabidhiwa wadhifa huo.

"Muungano wa Kenya African National Union (KANU) unapendekeza na kuwasilisha jina la Stephen Kalonzo Musyoka kama mgombeaji anayependekezwa kwa nafasi ya Naibu Rais katika Uchaguzi Mkuu ujao. Ni maoni yetu, na tunaamini kwa dhati kwamba Stephen Kalonzo analingana na mswada huo na ndiye anayefaa zaidi kuwa naibu Raila Amolo Odinga.," Taarifa ya Moi ilisoma.

IEBC iliwapatia wagombea urais wote hadi Mei 16 kuwa wamefanya uamuzi wa wagombea wenza wao na kuwasilisha majina.