Mkutano wa baraza la mawaziri ulikuwa mtego dhidi ya Ruto, Mudavadi adai

Muhtasari

• Mudavadi alidai kwamba mkutano wa baraza la mawaziri ulilenga kumdhalilisha Ruto lakini “kwa sababu naibu rais ni mwerevu aliamua kuhudhuria bila matarajio yao”.

• “Ruto ni mwerevu na anajua hata wakiitisha cabinet baada ya miaka mbili ati wajaribu kusafisha vitu, Ruto atajua vile atazungumza huko ili asihusishwe na matope ya watu wengine,” Mudavadi alisema.

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi
Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi Kinara wa ANC Musalia Mudavadi
Image: Musalia mudavadi/TWITTER

Mkutano wa baraza la mawaziri uliyofanyika siku ya Alhamsi chini ya uwenyekiti wa rais Uhuru Kenyatta ulikuwa mtego dhidi ya naibu rais William Ruto.

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi anadai kwamba mkutano huo wa baraza la mawaziri ulilenga kumdhalilisha Ruto lakini “kwa sababu naibu rais ni mwerevu aliamua kuhudhuria bila matarajio yao”.

 “Ruto ni mwerevu na anajua hata wakiitisha cabinet baada ya miaka mbili ati wajaribu kusafisha vitu, Ruto atajua vile atazungumza huko ili asihusishwe na matope ya watu wengine,” Mudavadi alisema.

Mudavadi aliendelea kusema “...Kwa sababu huu ulikuwa mtego walitaka kusema tuliitisha mkutano lakini yeye hakuja”.

Mudavadi anadai kwamba mkutano wa baraza la mawaziri uliitishwa baada ya rais Kenyatta na wandani wake kushtuka walipoambiwa kwamba wamekuwa wakimlaumu naibu rais kwa utendakazi duni na ilhali hawajakuwa wakifanya mikutano ya baraza la mawaziri kama inavyotakikana.

Alisema waandalizi walishtuka na kuitisha mkutano ya baraza la mawaziri haraka ili kufumba wakenya macho baada ya viongozi wa Kenya Kwanza kumsuta rais kwa kuendesha serikali bila mikutano ya baraza la mawaziri.

Kinara wa ANC alisema serikali imefanya maamuzi mengi bila idhini ya baraza la mawaziri.

Kulingana na Mudavadi muda umeyoyoma na rais Uhuru Kenyatta hawezi sasa kubadilisha jambo lolote.

“Kama hukulifanya katika kipindi cha miaka 10 iliyopita huwezi kulifanya katika miezi mitatu ya mwisho,” Mudavadi alisema.

Kinara huyo wa ANC alikuwa akihutubia wapiga kura kutoka eneo bunge la Lang’ata siku ya Alhamisi.

Mudavadi aliwasihi wakenya kumpigia kura naibu rais William Ruto na kujitenga na Raila Odinga ambaye alisema ni mradi wa rais Uhuru Kenyatta, huku akilenga kuendeleza uongozi wake kupitia kwa Raila.