Bahati kuwania kiti cha ubunge wa Mathare kwa tikiti ya Jubilee

Muhtasari
  • Kioni alisema chama hicho kilikuwa na masilahi ya vijana moyoni na hivyo kuamua kurejesha cheti cha Bahati
Kevin Bahati
Image: WILFRED NYANGARESI

Mwanamuziki Kevin Kioko almaarufu Bahati sasa atawania kiti cha ubunge cha Mathare baada ya Chama cha Jubilee kufanya mabadiliko katika uamuzi wake wa kuondoa cheti chake cha uteuzi.

Tangazo hilo lilitolewa na Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, wakati wa kikao na wanahabari katika makao makuu ya chama hicho jijini Nairobi.

Kioni alisema chama hicho kilikuwa na masilahi ya vijana moyoni na hivyo kuamua kurejesha cheti cha Bahati.

Kiti cha ubunge cha Mathare kilitengwa kwa ajili ya chama cha ODM.

Uamuzi huo ulizua ghadhabu miongoni mwa wagombea ambao walikuwa wakitazama viti mbalimbali vya kuchaguliwa lakini walifungiwa nje kwa sababu ya kupangiwa maeneo.

Haya yanajiri wiki chache baada ya msanii huyo kukejeliwa sana mitandaoni baada ya kulia akiwahotubia wanahabari, sababu ya kunyang'anywa cheti cha chama hicho.