Raila amtangaza Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake

Karua pia atakuwa waziri wa masuala ya haki na katiba.

Muhtasari

•Raila alisema alihitaji naibu ambaye ataangazia kushirikiana naye katika kazi za serikali ila sio ambaye atashindana naye.

•Kalonzo Musyoka na Gideon Moi walisusia mkutano huo wa KICC na badala yake kuandaa mkutano mbadala katika ofisi za SKM Command Centre mtaani Karen.

Raila Odinga na kiongozi wa Narc Martha Karua
Raila Odinga na kiongozi wa Narc Martha Karua
Image: FACEBOOK// MARTHA KARUA

Hatimaye mpeperusha bendera wa Muungano la Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga amemtangaza Martha Karua kama mgombea mwenza wake.

Raila alifanya matangazo hayo yaliyokuwa yamesubiriwa na wengi Jumatatu alasiri mbele ya maelfu ya wafuasi wake waliokuwa wamejumuika nje ya ukumbi wa KICC. Aliwasili katika ukumbi wa KICC mwendo wa saa saba kasorobo na kutoa hotuba yake takriban nusu saa baadae.

Raila alianza kwa kusoma majina 11 ya viongozi waliowasilisha ombi la kukabidhiwa wadhifa wa mgombea mwenza wake. Baadae aliendelea kusoma historia ndefu ya kazi muhimu ambazo Karua amewahi kufanyia taifa la Kenya.

"Baada ya kushauriana kwa kina tulikubaliana kuwa atakayeshikilia wadhifa wa naibu rais ni sharti awe mwanamke. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya historia inatuita tuangazia haki za wanawake.. Kwa heshima kubwa ningetaka kutangaza mgombea wangu na waziri wa masuala ya haki na katiba, Martha Wangari Karua  ," Raila alisema.

Karua alikuwa amependekezwa  na maelfu ya Wakenya pamoja na kundi kubwa la viongozi kuwa mgombea mwenza wa kinara huyo wa ODM katika kinyanganyiro cha Agosti 9.

Raila alisema alihitaji naibu ambaye ataangazia kushirikiana naye katika kazi za serikali ila sio ambaye atashindana naye.

Jumapili wiki iliyopita wzee kutoka jamii ya Kikuyu walimpendekeza kiongozi huyo wa Narc Kenya kuwa mgombea mwenza wa Raila.

Jopo la kuteua mgombea mwenza wa Azimio pia liliwahoji magavana Charity Ngilu (Kitui), Hassan Joho (Mombasa), Lee Kinyanjui (Nakuru) na Wycliffe Oparanya (Kakamega) na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Wengine ni pamoja na Mwakilishi wa Wanawake wa Murang'a Sabina Chege, Waziri wa Kilimo Peter Munya na aliyekuwa Mbunge wa Emgwen Stephen Tarus.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa KANU Gideon Moi walisusia mkutano huo wa KICC na badala yake kuandaa mkutano mbadala katika ofisi za SKM Command Centre mtaani Karen.

Kalonzo alipewa wadhifa wa mkuu wa mawaziri katika serikali ambayo Raila anakusudia kuunda.