Aisha Jumwa atofautiana vikali na DP Ruto

Muhtasari
  • Akizungumza katika kikao cha wanahabari, alisema pia hawatakubali kuachia PAA kiti chochote katika kaunti hiyo

Mzozo umeibuka katika Kaunti ya Kilifi, kuhusu usimamizi wa kampeni za urais za Naibu Rais William Ruto, saa chache baada ya Gavana Amason Kingi kutangazwa kuwa mmoja wa waratibu wa kampeni hizo Pwani.

Viongozi wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA) tawi la Kilifi, wamesisitiza kampeni hizo zinafaa ziendelee kusimamiwa na afisi ya chama hicho ambayo imekuwa ikipokea ufadhili kutoka kwa chama na Muungano wa Kenya Kwanza.

Afisi hiyo imekuwa ikiongozwa na Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, akisaidiana na wanachama wengine wa UDA akiwemo mwenzake wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya.

"Tunahofia kwamba rekodi yake mbaya itaathiri umaarufu wa UDA katika kaunti endapo hataitakatisha nadfi yake kwa wenyeji wa Kilifi. Mratibu wa UDA katika Kaunti ya Kilifi ni Aisha Jumwa na atasaidiwa na Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya. Wenyeji wa Kilifi bado wana wasiwasi kuhusu jinsi Kingi alitekeleza jukumu lake kama gavana wa kaunti hii. Kwa sababu hii, ili kujumuisha kura nyingi ambazo Naibu Rais William Ruto angepata Kilifi, tunamwomba aanze kupenya katika maeneo ya Kilifi huku akijisafisha,” mbunge huyo alisema. 

Akizungumza katika kikao cha wanahabari, alisema pia hawatakubali kuachia PAA kiti chochote katika kaunti hiyo.