Wagombea urais 55 watazamia kuwa debeni mnamo Agosti 9

Muhtasari

•Kinara wa ODM Raila Odinga ndiye mgombea urais pekee ambaye atatumia tikiti ya Muungano kuwania wadhifa huo.

•IEBC pia imetangaza kuwa wagombea ugavana 244 pia waliwailisha majina yao kwa tume kabla ya makataa. 

IEBC/Twitter
IEBC/Twitter
Image: Wafula Chebukati

Jumla ya Wagombea Urais hamsini na watano watakuwa kwenye debe katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, tume ya IEBC imetangaza.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, IEBC ilimetangaza kuwa wagombea urais 14 watapeperusha bendera ya vyama tofauti, wengine 40 ni wagombea huru huku mmoja tu akiwania wadhifa huo kwa tikiti ya Muungano.

Kinara wa ODM Raila Odinga ndiye mgombea urais pekee ambaye atatumia tikiti ya Muungano kuwania wadhifa huo. Ni rasmi kuwa naibu rais William Ruto atatumia tikiti ya chama chake cha UDA ila sio tikiti ya muungano wa Kenya Kwanza.

IEBC pia imetangaza kuwa wagombea ugavana 244 pia waliwailisha majina yao kwa tume kabla ya makataa. 

167 kati yao watawania wadhifa huo kwa tikiti za vyama mbalimbali huku wengine 77 wakiwa wagombea huru.

"Wagombea urais na ugavana watapitishwa kama wagombeaji na Msimamizi wa Uchaguzi wa Rais na Wasimamizi wa Uchaguzi wa Kaunti mtawalia wakati wa usajili mara tu baada ya sifa zao za kugombea katika nyadhifa husika kuthibitishwa," Taarifa iliyotiwa saini na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati ilisoma.

IEBC pia imetangaza kuwa wagombea urais na ugavana wataidhinishwa na kusajiliwa na Wasimamizi wa Uchaguzi wa Tume kati ya Mei 29 na Juni 7, 2022.

Kabla ya usajili, wagombea nyadhifa hizo watashiriki mikutano na wasimamizi wa uchaguzi ili kufahamishwa kuhusu mahitaji na utaratibu wa usajili wa mgombea.

Wagombea urais wote au wawakilishi wao wanatarajiwa kuhudhuria mkutano ambao utafanyika Bomas of Kenya mnamo Mei 23, 2022.

Wagombea viti vingine watafahamishwa kuhusu tarehe za mikutano yao na wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo yao.

"Tume inawataka wanaowania kufahamu mahitaji ya kusajiliwa kama wagombeaji kwa kufanya uchunguzi katika afisi za Kaunti na Maeneo Bunge ya Tume," Taarifa hiyo imesema.

Wagombea urais wamekumbushwa kuwa tayari na orodha ya angalau wafuasi 2000 wanaowaunga mkono.

Wagombea urais na ugavana ambao wana digrii kutoka vyuo vya nje ya nchi pia wamehitajika kufika kwenye afisi za Tume ili vyeti vyao  kuidhinishwa.