DP Ruto aahidi kutengenezea wakazi wa Eldoret nafasi 50,000 za kazi

Muhtasari

•Ruto pia ameahidi kuwa serikali yake  itatengeneza nyumba 10,000 za bei ya chini kwa wakazi wa Eldoret. 

•Ruto pia aliahidi kushughulikia mizozo ya muda mrefu ya umiliki wa ardhi katika eneo la Langas ambapo wakaazi hawana hati miliki. 

Image: FACEBOOK// WILLIAM RUTO

Naibu Rais William Ruto ameahidi kuwaundia wakazi wa kaunti ya Uasin Gishu nafasi za kazi 50,000 iwapo timu yake ya Kenya Kwanza itashinda katika uchaguzi wa Agosti 9. 

Ruto pia ameahidi kuwa serikali yake  itatengeneza nyumba 10,000 za bei ya chini kwa wakazi wa Eldoret. 

DP vilevile ameahidi kuteua mbunge wa ziada katika kaunti hiyo pamoja na MCAs wawili kutoka jamii za Waluo na Waluhya. 

Naibu rais alikuwa akizungumza katika eneo la Langas, mjini Eldoret, baada ya kuhudhuria ibada katika kanisa la PCEA Langas.

Aliwafanyia kampeni walioteuliwa na UDA katika eneo hilo akiwemo mbunge wa eneo hilo Oscar Sudi na gavana Jackson Mandago miongoni mwa wengine. 

Aliwataka wakazi kuwapigia kura wateule wote wa UDA ili kurahisisha kazi yake iwapo atachaguliwa kuwa rais mwezi Agosti

 "Ninataka kuwaahidi kwamba sitawaangusha na kama watu wangu hapa nyumbani, mtu asije hapa kuwapanga," Ruto alisema. 

Alisema Kenya Kwanza itapatia kipaumbele upanuzi wa uchumi kwa kuwekeza zaidi ya Sh100 bilioni ili kuunda nafasi nyingi za kazi kwa vijana.

  Ruto alisema Kenya itasalia na amani licha ya kampeni za kisiasa zinazoendelea.

Alipuuzilia mbali muungano wa Azimio huku akisema hauna mpango na viongozi wake wanapanga kufufua BBI ili kujiundia nyadhifa.

 "Kwetu sisi, kazi yetu ya kwanza itakuwa uchumi na ajira kwa vijana wetu," Ruto alisema.

 Naibu rais alisema wao kama viongozi wa Kenya Kwanza wameweka imani yao kwa Mungu kabla ya uchaguzi. 

Alisema alisoma katika Shule ya Upili ya Wareng eneo la Langas na kutembelea eneo hilo ni kama kurudi nyumbani. 

"Nilienda shule hapa Langas. Langas ni Jerusalem yangu," Ruto alisema. 

Ruto pia aliahidi kushughulikia mizozo ya muda mrefu ya umiliki wa ardhi katika eneo la Langas ambapo wakaazi hawana hati miliki. 

Alikuwa ameandamana na Moses Kuria, Ndindi Nyoro, Didmus Barasa na Kimani Ngunjiri, Oscar Sudi na Jackson Mandago miongoni mwa wengine. 

Sudi alisema uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa amani zaidi kwa sababu wakaazi wa eneo hilo walikuwa na umoja.

 Nyoro alimtahadharisha Rais Kenyatta kutomfanyia kampeni mgombea urais wa Azimio kwa sababu ataaibika kwenye kura. 

Alisema eneo la Mlima Kenya tayari limeamua kumuunga mkono Ruto mnamo Agosti 9. 

Alisema Ruto hata amepewa jina la utani Kamau katika eneo hilo kwa sababu walimchukulia kama mmoja wao. 

Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri alisema wanamuunga mkono DP Ruto kwa sababu ana uwezo wa kuunganisha nchi .

Alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kurudisha uungwaji mkono aliopokea kutoka kwa Ruto wakati wa uchaguzi uliopita. 

Mbunge Barasa aliwataka wakazi kutowapigia kura viongozi wa eneo hilo ambao wanamhujumu DP Ruto. 

Alimtaja mbunge wa Kesses Dkt Swarrup Mishra kuwa mmoja wa wanaofaa kukataliwa. 

Mishra anatetea kiti chake kama tikiti huru.