6 wakamatwa kwa kusababisha vurugu katika mkutano wa Karua Kirinyaga

Muhtasari
  • 6 wakamatwa kwa kusababisha vurugu katika mkutano wa Karua Kirinyaga
  • Sita hao wanasemekana kuupiga kwa mawe msafara wa Karua huko Kagumo na Kerugoya
Pingu
Image: Radio Jambo

Watu sita wamekamatwa kuhusiana na kisa cha hekaheka kilichoharibu mkutano wa mgombea mwenza wa Urais wa Azimio La Umoja Martha Karua kaunti ya Kirinyaga wiki jana.

Naibu kamishna wa Kaunti ya Kirinyaga ya Kati Daniel Ndege alithibitisha kukamatwa kwa watu hao siku ya Jumatatu.

Sita hao wanasemekana kuupiga kwa mawe msafara wa Karua huko Kagumo na Kerugoya.

“Juzi kuna baadhi ya watu walijaribu kuvuruga sheria na taratibu, wakati mmoja wa viongozi anarudi nyumbani, kuna baadhi ya watu walikodiwa na baadhi ya viongozi kurusha mawe na kumpigia kelele kiongozi huyo,” alisema.

"Hivi tunavyozungumza, kuna wavulana sita ambao wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuvuruga amani na kusababisha uhuni." Ndege aliwataka wakazi na wazazi kuwaongoza watoto wao dhidi ya kusababisha vurugu katika mikutano ya kisiasa.

"Ninawaomba wazazi kuwafahamisha watoto wao kwamba serikali haiwezi kuthubutu. Tukio hilo la machafuko liwe la kwanza na la mwisho. Yeyote atakayejaribu kufanya hivyo atakabiliwa na hasira kali ya sheria."

Wakati huohuo aliwanyooshea kidole baadhi ya wanasiasa wenye tabia ya kuwapa vijana fedha ili waweze kusababisha fujo katika mikutano ya wapinzani.

Ndege alisema kuna haja ya uvumilivu wa kisiasa nchi inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Kukamatwa kwa sita hao kunajiri wiki moja tu baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Karanja Kibicho kuwataka polisi kuwachukulia hatua kali watu wanaofanya mikutano ya kisiasa.