Gavana Mutua kuwania kiti cha ubunge cha Mwala? - Aweka mambo wazi

Muhtasari

•Mutua ameweka wazi kuwa hatagombea kiti chochote cha kisiasa katika uchaguzi wa mwaka mkuu.

•Madai yalichimbuka kuwa Mutua aliamua kuchukua hatua hiyo ili kujihakikishia mustakabali wa kisiasa.

GAVANA WA MACHAKOS ALFRED MUTUA
Image: WILFRED NYANGARESI

Gavana wa Machakos Alfred Mutua ametupilia mbali madai kuwa atakuwa anawania kiti cha ubunge cha eneo la Mwala katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Mutua ameweka wazi kuwa hatagombea kiti chochote cha kisiasa katika uchaguzi wa mwaka mkuu.

"Ili kuepusha mashaka, ningependa kufafanua kwamba kwa wakati huu, sigombei nafasi yoyote ya kuchaguliwa katika uchaguzi ujao," Mutua alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Gavana huyo wa muhula wa pili pia alithibitisha uaminifu wake katika Kenya Kwanza na kueleza kuwa kwa sasa anaangazia kampeni za muungano huo unaaongozwa na naibu rais William Ruto.

"Ninaangazia kupigia debe muungano wa Kenya Kwanza ili Kenya ipate mfumo mpya ambapo ndoto zinaweza kutimia," Alisema.

Uvumi kuwa gavana huyo anakusudia kuwania kiti cha ubunge cha Mwala ulienea sana mitandaoni siku ya Jumatatu.

Madai yalichimbuka kuwa Mutua aliamua kuchukua hatua hiyo ili kujihakikishia mustakabali wa kisiasa.

Orodha iliyodaiwa kutoka kwa IEBC ilionyesha jina la Mutua likiwa miongoni mwa wagombea viti vya ubunge katika kaunti ya Machakos.

Haya yanajiri wakati ambapo kuna tetesi nyingi kuhusu mipango yake ya kisiasa baada ya kustaafu kutoka kiti cha ugavana mnamo tarehe 9 Agosti.

Mnamo Mei 15, naibu rais William Ruto alimteua gavana huyo kuongoza kampeni za Kenya Kwanza katika eneo la Ukambani kwa ushirikiano na mwenyekiti wa UDA Johnstone Muthama.

Uteuzi huo ulikuja wiki moja tu baada ya kiongozi huyo wa Maendeleo Chap Chap kugura muungano wa Azimio la Umoja- One Kenya na kujiunga na Kenya Kwanza.