Mudavadi azungumzia njama ya rais Kenyatta na Raila iliyomsukuma kugura Azimio

Muhtasari

• Mudavadi amesema aligundua njama kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga ya kumtaka kuwa kibaraka kwenye harakati za kura za urithi wa Urais.

•Mudavadi amesema kuwa hakuna yeyote atakayetikisa ngome yake akidai kuwa chama cha ANC kitaibuka na idadi ya juu ya viongozi waliochaguliwa kuliko mwaka wa 2017.

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi
Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi Kinara wa ANC Musalia Mudavadi
Image: Musalia mudavadi/TWITTER

Kinara wa Chama cha ANC Musalia Mudavadi amesema kuwa aligundua njama kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga ya kumtaka kuwa kibaraka kwenye harakati za kura za urithi wa Urais wa 2022, na ndio sababu kuu ya yeye kuwachenga na kukwepa mtego wao ambao kwa sasa ndio mrengo wa Azimio.

Akizungumza kwenye ngome yake kuu ya Vihiga, alipokuwa akiwahutubia wenyeji wa eneo la Chavakali, Mudavadi amesema kuwa alivumbua msukumo wa Earth Quake, na kuchangia pakubwa kwenye msukumo wa kubuni mrengo wa Kenya Kwanza kwani alionelea kuwa upande wa pili ulikuwa na njama ya kuendeleza siasa za utapeli, uwongo na ukandamizaji ambao hautawafaidi wakenya.

Mudavadi akiwarai wenyeji wa eneo la magharibi mwa Kenya kuunga mkono vuguvugu la Kenya Kwanza akisema kuwa mkataba wa makubaliano kati ya vyama vya ANC, FORD-K na UDA pamoja na vyama vingine vilivyoungana na Kenya Kwanza, unawapa weneyeji wa magharibi mwa Kenya nafasi kubwa kwenye utawala wa Serikali ya Kenya Kwanza hasa kimaendeleo.

Amesema kuwa kwenye mkataba waliotia saini yeye na kinara wa FORD-K Moses Wetangula chini ya Kenya Kwanza ambayo mpeperushaji wa Bendera yake ni naibu wa rais William Ruto, unathamini kuangazia maendeleo hasa miundo msingi kama vile ujenzi wa barabara, ufufuaji wa viwanda kama vile Mumias Sugar, ufufuaji wa viwanda vyaa kahawa na majani chai pamoja na kuinua biashara katika eneo kuu la magharibi mwa Kenya.

Mudavadi aidha amesisitiza kuwa jamii ya eneo la magharibi mwa Kenya miaka nenda miaka rudi imekuwa ikimpigia debe kinara wa ODM Raila Odinga, lakini kwa sasa amesema kuwa Odinga na mrengo wake wa Azimio hawana lao kwani asilimia 90 na zaidi ya kura kutoka magharibi mwa Kenya wanajizatiti ziingie kwenye kapu la Kenya Kwanza.

Mudavadi akitetea mkataba wa Kenya Kwanza na kusema kuwa wana azimio wanapiga domo tupu ilhali hawawaelezii wenyeji wa magharibi ni nini watafanyia hasa kimaendeleo kwenye jitihada za kubadilisha maisha ya wenyeji wa eneo hilo.

Mudavadi pia amepigia debe chama chake cha ANC akisema kuwa kwenye ngome zake kuu ni lazima kiwike na kutwaa ushindi mkubwa. Alikuwa akipigia debe wagombeaji wa chama cha ANC hasa kutoka kaunti ya Vihiga ambako ni ngome yake kuu.

Mudavadi amesema kuwa hakuna yeyote atakayetikisa ngome yake akidai kuwa chama cha ANC kitaibuka na idadi ya juu ya viongozi waliochaguliwa kuliko mwaka wa 2017.

Mudavadi amesema kwenye meza ya mazungumzo ya Kenya Kwanza lazima aandamane na majeshi yake.

Vile vile kinara huyo wa ANC ambaye pia ni kigogo mkuu wa Kenya Kwanza, amekashifu njama za upande wa serikali unaounga mkono Azimio, kwa kuwashurutisha machifu na manaibu wao kuwarai wakenya kupigia kura upande wa Azimio. Akisema kuwa kuna njama ya kupinda mkondo wa haki kwenye zoezi la Agosti 9, huku akisema kuwa Kenya Kwanza ipo macho na hilo halitatimia.

Hii leo pia Mudavadi na kikosi cha Kenya Kwanza kutoka eneo la Magharibi walizuru pia maeneo ya Webuye kaunti ya Bungoma, Funyula kaunti ya Busia na kumalizia Luanda, Vihiga.