Tafadhali nisamehe- Ruto amsihi rais Kenyatta

Muhtasari

•Naibu rais William Ruto amemuomba msamaha rais Uhuru Kenyatta kwa kushindwa kutimiza matarajio yake.

• Ruto amemshukuru rais kwa kumpa fursa ya kuwa msaidizi wake katika kipindi cha takriban mwongo mmoja ambacho kimepita.

Naibu rais William Ruto
Naibu rais William Ruto
Image: EZEKIEL AMINGA

Naibu rais William Ruto amemuomba msamaha rais Uhuru Kenyatta kwa kushindwa kutimiza matarajio yake.

Akizungumza katika Mkutano wa Maombi  ya Kitaifa uliofanyika Safari Park Hotel Alhamisi asubuhi, Ruto alibainisha kuwa huenda hajatimiza matarajio ya rais katika kipindi ambacho amekuwa akihudumu kama naibu wake.

"Najua katika huduma yangu kama naibu rais huenda nimekosa kutimiza matarajio ya bosi wangu, mheshimiwa rais , rafiki yangu naomba msamaha," Ruto alisema.

DP alimshukuru rais  kwa kumpa fursa ya kuwa msaidizi wake katika kipindi cha takriban mwongo mmoja ambacho kimepita.

Mgombea urais huyo kwa tikiti ya UDA katika uchaguzi wa Agosti pia alimtakia rais Kenyatta mema anapoelekea kustaafu.

"Ni ombi langu kuwa Mungu atakupa kila utakacho moyoni na uweze kufurahia amani ya muda ambao Mungu atakupa. Hilo ndilo ombi langu," Alisema.

Mzozo kati rais Kenyatta na naibu wake ulijionyesha wazi tena katika hafla hiyo ya maombi ya taifa ya mwisho katika kipindi cha utawala wao.

Rais ambaye hapo awali aliketi katika meza moja na naibu wake pamoja na maspika wa Bunge la Kitaifa na Seneti aliketi katika meza tofauti.

Wakati huu, rais Kenyatta Uhuru aliketi katika meza yake na Jaji Mkuu Martha Koome na Mwanasheria Mkuu Paul Kihara.

DP amewataka Wakenya kusamehe uongozi wake na rais Kenyatta kwa matarajio ambayo huenda wameshindwa kuyatimiza.

"Najua tumejaribu kadri ya uwezo wetu. Huenda tumekosa kama mlivyotarajia. Tumewaangusha katika mambo fulani. Hatujakuwa na maarifa kama tulivyohitajika kuwa. Tumefeli katika mambo fulani. Naomba msamaha wenu," Ruto alisema.

Ruto pia alitangaza kuwa amewasamehe viongozi na wananchi wote ambao wamewahi kumkosea. Alisema matakwa yake ni watu waelekee kwenye uchaguzi ujao bila chuki yoyote dhidi ya wenzao.