IEBC yamwidhinisha mkurugenzi mtendaji wa Keroche Tabitha Karanja kuwania kiti cha Seneti Nakuru

Muhtasari
  • IEBC yamwidhinisha mkurugenzi mtendaji wa Keroche Tabitha Karanja kuwania kiti cha Seneti Nakuru
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia ya Keroche, Tabitha Karanja akihutubia wanahabari kuhusu kufungwa kwa kampuni hiyo na KRA kutokana na kutolipa ushuru
Image: FREDRICK OMONDI

Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa Keroche Breweries Limited Tabitha Karanja Keroche ameidhinishwa rasmi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwania kiti cha useneta wa Nakuru mnamo Agosti.

Bi Karanja alitoa tangazo hilo kwenye mtandao wake wa kijamii siku ya Jumanne huku akipongeza tume hiyo kwa kufaulu kupitia mchujo.

“Leo nimeidhinishwa rasmi na afisi ya @IEBCKenya Kaunti ya Nakuru kama mgombeaji useneta chini ya Muungano wa UDA Kenya Kwanza. Hii ni ya kushukuru IEBC kwa mchakato mzuri ambao ulikuwa wa kina na wa kirafiki,” Keroche aliandika kwenye Twitter.

Mwaniaji huyo wa useneta anayewania kiti cha useneta chini ya Naibu Rais William Ruto anayeongoza  chama cha United Democratic Alliance (UDA) awali alienguliwa kutoka kwa mchakato huo kwa kukosa stakabadhi zinazohitajika kwa zoezi hilo.

Siku ya Jumatatu, alishindwa kuwasilisha cheti chake cha uteuzi wa UDA na pia alikuwa na kigugumizi baada ya kufanya ‘malipo ya ziada’ kwa tume.