Chebukati apuuzilia mbali madai ya Ruto kuhusu sajili ya wapiga kura

Muhtasari

• Chebukati alisema majina milioni moja yanayodaiwa kukosekana ni ya wapiga kura waliotuma maombi ya uhamisho.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) WAFULA CHEBUKATI
Image: EZEKIEL AMING'A

Mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi na mipaka (IEBC) Wafula Chebukati amewahakikishia Wakenya kwamba hakuna majina ambayo yameondolewa kutoka sajili za wapiga kura kama alivyodai Naibu Naibu Rais William Ruto.

Akiwahutubia wanahabari katika eneo la Bomas siku ya Alhamisi, Chebukati alisema majina milioni moja yanayodaiwa kukosekana ni ya wapiga kura waliotuma maombi ya uhamisho.

"Wanaoeneza uvumi kuwa daftari la data limepotea wafahamishwe kuwa liko shwari. Hakuna muingilio wa aina yoyote katika mifumo tunayotumia kutunza rejista," alisema.

"Tutawajibika kwa kila Mkenya aliyejiandikisha kupiga kura."

Alisema jambo hili linaweza pia kutokea kutokana na kufutwa kwa baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Alisema tume hiyo itaidhinisha sajili ya mwisho na kuitangaza katika gazeti la serikali kufikia Juni 9 na kisha itagawanywa katika kwa kila kaunti, maeneo bunge na wadi.

Alidokeza kuwa rejista za wapiga kura zitapatikana kwa wapiga kura wote kuangalia maelezo yao hadi siku saba hadi tarehe 9 ya uchaguzi.

Mwenyekiti huyo wa IEBC alisema tume hiyo imesajili wapiga kura milioni 22.5 na sajili hiyo inafanyiwa ukaguzi na kampuni ya kimataifa ya KPMG.

"Tume inawahakikishia Wakenya kwamba sajili iko imara na taratibu zinazoendelea ni kuhakikisha sajili ni safi tayari kwa uchaguzi," alisema.

Chebukati aliongeza kuwa ukakuzi wa sajili utakuwa mchakato wa uwazi ambapo kila mtu ataweza kuona ni wapi atapiga kura yake.