EACC yataka wagombea viti 241, wakiwemo 2 wa urais kuzuiwa kushiriki uchaguzi wa Agosti 9

Muhtasari

•EACC inataka wagombea viti hao kufungiwa nje ya uchaguzi wa Agosti 9 kwa sababu zinazohusiana na ufisadi.

•Mwangi wa Urais wa chama  cha Usawa Kwa Wote Mwangi Wa Iria ni miongoni mwa wagombea urais ambao EACC inataka wafungiwe nje ya kinyang'anyiro hicho.

Picha ya makao makuu ya EACC jijini Nairobi
Picha ya makao makuu ya EACC jijini Nairobi
Image: MAKTABA

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imewataja wagombea viti mbalimbali vya kisiasa 241 kama watu wasiofaa kuwania nyadhifa za umma.

EACC inataka wagombea viti hao kufungiwa nje ya uchaguzi wa Agosti 9 kwa sababu zinazohusiana na ufisadi.

Tume hiyo ya kupambana na ufisadi imesema orodha hiyo imetokana na mchakato wa uhakiki wa uadilifu ambao walifanya kuhusu watu 21,863 wanaoomba kusajiliwa kama wagombea wa nyadhifa mbalimbali za kisiasa.

"EACC inawachukulia watu hawa kuwa wamekosa kufuata viwango vya maadili vilivyowekwa kwa ajili ya kuchaguliwa katika ofisi za umma. EACC inatumai kuwa IEBC itafanya maamuzi yanayofaa kwa kuongozwa na Maadili ya Kikatiba na maslahi ya umma."

Katika barua kwa IEBC, EACC inataka wawaniaji 2 wa urais na mgombea mwenza mmoja kunyimwa kibali. Wagombea 54 walikuwa wameonyesha azma ya kugombea urais.

Mwangi wa Urais wa chama  cha Usawa Kwa Wote Mwangi Wa Iria ni miongoni mwa wagombea urais ambao EACC inataka wafungiwe nje ya kinyang'anyiro hicho.

"Tume ilipokea na kuchunguza madai ya kuzuia wachunguzi wa EACC na uharibifu wa ushahidi wakati wa kutekeleza hati ya upekuzi. Uchunguzi ulibaini kuwa Mgombea huyo alikuwa na hatia," EACC ilisema kuhusu Wa Iria kutostahili kushiriki.

Justus Zachous Onyango Juma ambaye anawania urais kwa tikiti ya Justice and Freedom Party pia ameshindwa mtihani wa uadilifu wa EACC.

Mgombea mwenza wa Urais wa Chama cha Republican Matayo Jared Obwogi pia ametajwa katika orodha hiyo ya EACC.

Jumla ya wagombeaji 61 wa ugavana na naibu gavana pia wamenyooshewa vidole na tume hiyo.

Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru na Waliokuwa Magavana wa Nairobi Evans Kidero na Mike Mbuvi Sonko ni miongoni mwa majina mashuhuri ambayo EACC imetaka wazuiwe kuwania viti vya ugavana.

Kidero anamezea mate kiti cha ugavana cha Homa Bay huku Sonko akitazamia kuchukua usukani wa Mombasa.

Gavana wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki pia ameshindwa katika mtihani wa uadilifu wa EACC.

Kwa wanaowania viti vya Seneti, EACC inataka IEBC kuwazuia Gavana wa Migori Okoth Obado (Migori), Mbunge wa Kitutu Chache Richard Onyonka (Kisii), Paul Karungo Thangwa (Kiambu), Mbogo Lilian Muthoni Wanjiru (Embu), Chelumo Benjamin Kai (Kilifi) na Mungata Danson Buya (Tana River) kutoka kuwania.

Mwakilishi wa Wanawake wa Uasin Gishu Gladys Boss Shollei pia ameorodheshwa kama wale ambao hawafai kupitishwa katika orodha ya wanasiasa 19 walioorodheshwa katika kitengo cha wawakilishi wa Wanawake.

EACC wakati huo huo imeripoti jumla ya wagombea 58 wanaotaka kuchaguliwa kuwa Wabunge wa bunge la kitaifa.

Miongoni mwao ni Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi, Gavana wa Busia Sospeter Ojamong (Teso Kusini), Mbunge wa Sirisia John Waluke, Samuel Arama (Nakuru Mashariki), Gavana Alfred Mutua Nganga (Mwala) na Mbunge Alfred Keter (Nandi Hills) miongoni mwa wengine.

EACC pia imeorodhesha wagombea viti vya MCAs 94 ambao inataka wazuiwe kuwania wadhfa huo.