Mpiga kura ataka Malala azuiwe kwenye kinyang'anyiro cha ugavana kwa madai ya karatasi za masomo

Muhtasari
  • Mpiga kura ataka Malala azuiwe kwenye kinyang'anyiro cha ugavana kwa madai ya karatasi za masomo
Seneta wa Kakamega Cleopas Malala
Image: MAKTABA

Mpiga kura wa Kakamega amehamia kortini akitaka IEBC kutomwidhinisha mgombea wa ugavana wa Kakamega Cleophas Malala, akidai hana cheti cha digrii.

Fred Muka anadai kuwa shahada ya Malala inayodaiwa kuwa ya USIU si ya kweli kwa hivyo hastahili kuwania nafasi ya Ugavana.

Kupitia wakili Duncan Okatch, Muka ameendelea kusema cheti cha mbunge huyo wa KCSE kutoka Shule ya Upili ya Kamusinga pia si ya kweli.

Muka anadai Malala hana karatasi zinazohitajika ili kuwania kiti cha Ugavana wa Kakamega.

Kulingana na karatasi za mahakama, cheti cha shahada ya USIU cha Malala kina kutofautiana, dosari na ukinzani ambazo zinafanya kuamini kuwa si halisi.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, Seneta Malala alipewa jukumu la kueleza kwa nini cheti chake kilisomwa 2019 lakini anadai kuwa alihitimu kati ya 2010 na 2011.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga, seneta huyo alijitahidi kukumbuka tarehe na mwaka kamili wa kuhitimu kwake, akipuuza maswali kutoka kwa mwandishi wa habari ambaye alitaka ufafanuzi juu ya tarehe zinazokinzana.

"Ndio nakuambia kama hukufanya degree huwezi jua," Malala alisema.

Malala ambaye anawania kiti cha ugavana wa Kakamega kwa tiketi ya chama cha ANC katika uchaguzi wa Agosti 9, amekuwa akipambana na madai ya kughushi vyeti vyake vya masomo.

Ili mtu afuzu kwa nafasi ya ugavana wa kaunti nchini Kenya, lazima miongoni mwa wengine; kuwa mwenye shahada kutoka Chuo Kikuu kinachotambuliwa nchini Kenya.