Nimerudi, jiandae kuenda nyumbani!- Kalonzo amwambia Ruto

Muhtasari

•Kalonzo alisema alikuwa amechukua mapumziko na sasa yuko tayari kuongoza kampeni  zitakazomfanya Ruto kurejea nyumbani katika raundi ya kwanza ya uchaguzi.

•Kalonzo alisema serikali ya Raila itakuwa mahali salama kwa utawala wa sheria, uhuru wa mfumo wa mahakama na mahitaji ya raia.

Kalonzo Musyoka akihutubia waandishi wa habari mnamo Alhamisi.
Kalonzo Musyoka akihutubia waandishi wa habari mnamo Alhamisi.
Image: WILFRED NYANGARESI

Alhamisi Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alimtupia vijembe Naibu Rais William Ruto huku akimwambia ajiandae kurudi nyumbani baada ya uchaguzi wa Agosti.

Akizungumza katika mkutano wa kwanza wa pamoja na kinara wa ODM Raila Odinga baada ya kujiunga tena na Azimio, Kalonzo alisema wako tayari kufanya kampeni kama timu.

Kiongozi huyo wa Wiper alisema alikuwa amechukua mapumziko kutoka kwa siasa na sasa yuko tayari kuongoza kampeni ambazo zitamfanya Ruto na timu yake kurejea nyumbani katika raundi ya kwanza ya uchaguzi.

"Nilikuwa nikipumzika. Raila alikuwa ameniweka kama kipuri. Sasa nimerejea. Mimi ndiye Messi wa timu hii, narudi kuleta ushindi," aliongeza.

Alizungumza huko Mukuru Kwa Njenga, Nairobi, ambapo mkutano wa kwanza wa pamoja ulifanyika.

Kalonzo alidhihirisha imani kuwa timu yao sasa ni timu ya kutisha ambayo itatoa ushindi bila hitaji la Rais Uhuru kujikita katika kampeni.

"Namuunga mkono wangu Uhuru Kenyatta. Ameonesha hataki kufanya Raila mradi...Tunamwambia apumzike, wacha Martha Karua na Raila na Kalonzo waokoe Kenya hii kutokana na ufisadi," alisema.

Kalonzo alisema serikali ya Raila itakuwa mahali salama kwa utawala wa sheria, uhuru wa mfumo wa mahakama na mahitaji ya raia, kutokana na ukweli kwamba kuna mawakili wawili wakuu katika afisi kuu.

Zaidi ya hayo, kiongozi huyo wa Wiper alisema Uhuru ni kiongozi mzuri ikizingatiwa kwamba tayari ameonyesha nia ya kuondoka mamlakani baada ya muhula wake kukamilika.

"Afrika inakabiliwa na matatizo ya uongozi. Sio viongozi wengi walio tayari kujiuzulu kama Uhuru ambaye amemuidhinisha Raila kushika wadhifa huo. Hili ni jambo la kushangaza si kwa Kenya pekee bali pia Bara la Afrika."