DP Ruto hatimaye aidhinishwa kuwania urais na IEBC

Muhtasari

•Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alitangaza hayo Jumamosi baada ya Ruto na mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua kuwasilisha stakabadhi zinazohitajika.

•Kwa vyombo vya habari, DP alisema ni wakati wao kuwa waadilifu na wenye usawa wakati wa kuripoti kampeni za kisiasa kabla ya uchaguzi.

Naibu rais William Ruto
Naibu rais William Ruto
Image: EZEKIEL AMINGA

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)imemuidhinisha mgombea urais wa UDA William Ruto kuwania urais katika uchaguzi wa Agosti 9.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alitangaza hayo Jumamosi katika ukumbi wa Bomas of Kenya baada ya Ruto na mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua kuwasilisha stakabadhi zinazohitajika.

"Ombi la William Ruto na mgombea mwenza kushiriki uchaguzi wa urais wa Agosti limeidhinishwa. Sasa nitawakabidhi cheti cha usajili," Chebukati alisema huku shangwe na nderemo kutoka kwa wafuasi wa Ruto na viongozi wa Kenya Kwanza walioandamana naye hadi Bomas zikishamiri hewani.

Naibu Rais William Ruto aliishukuru IEBC kwa jukumu lao la kuhakikisha Wakenya wanafanya uchaguzi wa kuaminika na kuwataka wawe waadilifu wanapotekeleza majukumu yao.

"Nimefurahi kupata cheti kitakachoniwezesha mimi na naibu wangu kushiriki katika uchaguzi wa Agosti. Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejitolea kwa maadili tuliyotia saini... Tuna imani upo kwenye kazi na tutafanya kazi nanyi kwa bidii," alisema.

Kwa vyombo vya habari, DP alisema ni wakati wao kuwa waadilifu na wenye usawa wakati wa kuripoti kampeni za kisiasa kabla ya uchaguzi.

"Ni jambo la heshima zaidi kufanya. Tumeeleza wasiwasi huu. Pia tunawasihi (IEBC) muwahudumie wagombeaji wote katika kinyang'anyiro hiki kwa usawa," akasema.

"Tunaomba tu kutendewa haki... Tutashirikiana na Wakenya wote katika uchaguzi huu," alisema na kuwataka Wakenya kusalia na amani wakati wa kuandaa uchaguzi.

Baada ya kuwasilisha karatasi zake, Ruto ataingia jijini kuzuru mitaa mbalimbali jijini Nairobi kisha amalizie katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji lililo eneo bunge la Kamukunji.

Atakuwa akijipigia debe na vilevile kuwafanyia kampeni wagombeaji wake wa Kenya Kwanza wakati wa ziara yake.

Msafara wa Ruto utasimama angalau katika vituo saba ambapo atauza mtindo wake wa kiuchumi wa chini kwenda juu.

Ataanzia South C, South B, Mukuru, City Stadium, Gikomba, Majengo na hatimaye Kamukunji.