Sonko akataliwa na IEBC, alipowasilisha stakabadhi zake

Muhtasari

•  IEBC ilifahamisha gavana huyo wa zamani kwamba hangeweza kuidhinishwa kwa vile shahada yake haikuwa imeidhinishwa na Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu. 

•  Sonko ambaye anapeperusha bendera ya Wiper Party analenga kumrithi Gavanana Hassan Joho anaeondoka baada ya kukamilisha kipindi cha mihula miwili.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Image: Facebook// Mike Sonko

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko amenyimwa cheti cha kuwania kiti cha ugavana wa Mombasa. 

Tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) ilitaja kuondolewa kwake ofisini kupitia kura ya kutokuwa na imani naye katika bunge la kaunti ya Nairobi kama sababu kuu iliyomfanya asipewe kibali cha kuwania urais. 

Wakati uo huo, IEBC ilifahamisha gavana huyo wa zamani kwamba hangeweza kuidhinishwa kwa vile shahada yake haikuwa imeidhinishwa na Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu. 

Kauli hiyo ya ilizua hali ya mshikemshike katika afisi za IEBC huku Sonko akijaribu kushawishi maafisa wa IEBC kuidhinisha uteuzi wake. 

Mgombea huyo wa ugavana alikuwa amefika katika Chuo cha mafunzo ya Serikali (KSG) ili kupata kibali cha IEBC. 

Sonko ambaye anapeperusha bendera ya Wiper Party analenga kumrithi Gavanana Hassan Joho anaeondoka baada ya kukamilisha kipindi cha mihula miwili.  

Aliandamana na mgombea mwenza wake Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo na aliyekuwa mbunge wa Matuga Chirau Mwakwere. Siku ya Jumamosi, IEBC ilitangaza kumzuia Sonko kuwania kiti cha ugavana wa Mombasa kwa misingi ya sheria.

 Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema Gavana wa Nairobi aliyetimuliwa hakufaa kuwania kiti hicho katika uchaguzi wa Agosti.

 Alisema Tume ya IEBC ilikuwa imepokea ripoti kutoka kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi iliyoorodhesha mwaniaji mmoja wa ugavana, mwaniaji mmoja wa useneta na mgombeaji mmoja wa Bunge la Kaunti kuwa hawafai kushikilia nyadhifa za umma kufuatia kutimuliwa kwao.

 Lakini Sonko alidai kuwa Katiba ya Kenya haisemi wazi kwamba wawaniaji walio na kesi zozote mahakamani wamezuiwa kuwania viti katika chaguzi.