Wakenya watoa hisia mseto baada ya Igathe kuonekana akiosha vyoo vya umma Nairobi

Muhtasari

•Igathe amekuwa akizamia mitaani na kuungana na wakazi katika kazi zao na pilkapilka zingine za kila siku.

•Amesema usimamizi wa vyoo vya umma jijini Nairobi utakuwa moja ya vipaumbele vyake ikiwa atatwaa ugavana.

Image: TWITTER// POLYCARP IGATHE

Mgombea ugavana wa Nairobi kwa tikiti ya Jubilee Polycarp Igathe ameendelea kuwashangaza Wakenya kwa njia zake za kipekee za kuwarubuni wapiga kura.

Igathe ambaye ndiye chaguo la Muungano wa Azimio la Umoja katika kinyang'anyiro cha Nairobi amekuwa akizamia mitaani na kuungana na wakazi katika kazi zao na pilkapilka zingine za kila siku.

Picha za mwanasiasa huyo akiosha vyoo vya umaa jijini zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii huku Wakenya wakizijadili na kutoa hisia tofauti.

"Tuna ukosefu mwingi wa vyoo vya umma jijini Nairobi. Ndiposa nimekuja hapa ili nionyeshe kuwa sio vyoo vya umma tu vinahitajika, lazima choo kiwe safi.Huu utakuwa mji safi na nitaendelea kufanya kazi kama mtu safi," Igathe alisema baada ya kuviweka chini vifaa vyake vya kuosha choo.

Alisema usimamizi wa vyoo vya umma jijini Nairobi utakuwa moja ya vipaumbele vyake ikiwa atatwaa ugavana.

"Kunapaswa kuwa na vyoo vingi vya umma katika maeneo ya soko, vituo vya mabasi na karibu na CBD ili kulinda usafi wa watu na mazingira. Nairobi itakuwa Jiji safi na inayong'aa!," Alisema kupitia Twitter.

Wanamitandao wameendelea kutoa maoni mbalimbali kufuatia kitendo cha mgombea ugavana huyo, baadhi wakionekana kuridhishwa huku wengine wakidai ni mojawapo ya mbinu nyingi ambazo wanasiasa hutumia kuwahadaa wapiga kura.

Haya ni baadhi ya maoni ya Wakenya kwenye Twitter:

@ItsMutai "Hii si PR tena. Hapana nakataa kufikiria kuwa hii ni PR. Mtu huyu anaelewa matatizo wanayokumbana nayo wapiga kura wake kuliko tulivyofikiri. Anaelewa kuungana na mpiga kura, lazima akutane naye kwenye makazi yake ya asili hata kwenye vyoo. Polycarp Igathe anaelewa biashara yake,

@osorojnr "Nani atamsimamisha Igathe?"

@Queens_ofRaila Lo! Mhe Polycarp Iganthe anaosha choo cha umma jijini Nairobi. Inatia motisha sana

Igathe mwenyewe medai kuwa vitendo vyake ni ishara tosha kuwa yeye ni kiongozi ambaye yupo tayari kuwatumikia wakazi wa Nairobi ikiwa atachaguliwa kuwa  gavana.

"Kiongozi hutumikia watu wake. Huwa najivunia kuwatumikia wakazi wa Nairobi na nitaendelea kuwatumikia nikichaguliwa kuwa gavana," Alisema kupitia Twitter.

Igathe anatazamia kuwa gavana wa nne wa Nairobi baada ya uchaguzi wa Agosti 9. Atakuwa anamenyana na wengine kama Johnstone Sakaja wa UDA na Agnes Kagure ambaye ni mgombea huru.