Marekani yahimiza uchaguzi huru na wa haki Kenya baada ya Ruto kuibua madai ya wizi wa kura

Muhtasari

•Blinken alisema Marekani ina furaha kwamba IEBC imeidhinisha wagombeaji wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9 nchini Kenya.

•Ruto alidai kuwa karibu wapiga kura milioni moja, hasa kutoka ngome zake, wameondolewa kwenye sajili la wapigakura.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akizungumza katika chumba cha muhtasari wa Wizara ya Mambo ya Nje huko Washington, Marekani Januari 7, 2022.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akizungumza katika chumba cha muhtasari wa Wizara ya Mambo ya Nje huko Washington, Marekani Januari 7, 2022.
Image: REUTERS

Marekani imetoa wito wa Kenya kufanya uchaguzi huru na wa haki baada ya wagombea wakuu kuibua maswali iwapo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka imejitayarisha vyema kusimamia uchaguzi wa kuaminika tarehe 9 Agosti.

Katibu wa Marekani Antony Blinken alisema Marekani ina furaha kwamba IEBC imeidhinisha wagombeaji wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9 nchini Kenya.

Blinken pia alipongeza mwanzo wa kampeni za uchaguzi  ujao hapa nchini.

"Kama nilivyomwambia Waziri wa Kenya Omamo mwezi uliopita, Marekani inasimama na Wakenya kuunga mkono uchaguzi huru, wa haki na wa amani," alisema.

Matamshi ya Blinken yanajiri siku chache baada ya Naibu Rais William Ruto kufanya mkutano na wajumbe wa Umoja wa Ulaya ambapo alidai kulikuwa na majaribio ya kuvuruga uchaguzi.

Wakati wa mkutano huo, mgombea urais huyo wa UDA alidai kuwa karibu wapiga kura milioni moja, hasa kutoka ngome zake, wameondolewa kwenye sajili la wapigakura kinyume cha utaratibu.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka(IEBC)  Wafula Chebukati alipuuzilia mbali madai hayo akisema "data za wapiga kura wote ziko sawa."

"Tusizungumzie kuhusu majina milioni moja kukosa, hakuna kitu kama hicho, hakipo," Chebukati alisema akijibu madai ya Ruto.

Ruto mnamo Alhamisi alidai kumekuwa na ufutaji uliotekelezwa na baadhi ya watendaji serikalini ambao wamedhamiria kudhoofisha uwezo wa IEBC kufanya uchaguzi wa kuaminika, wa uwazi na wa kidemokrasia.

“Nyinyi (wajumbe wa EU) mmeona kwenye vyombo vya habari kwamba kulikuwa na jaribio la kufuta majina kutoka kwa sajili ya IEBC na karibu majina 800,000 kwa namna fulani yametoweka kwenye sajili... Ni katika uwanja wa umma na nadhani hata IEBC imesema. wanafanya hatua za kurekebisha,” Ruto alisema.

Mgombea urais wa Azimio Raila Odinga pia aliitaka Tume hiyo kuhakikisha kuwa nchi inaandaa uchaguzi huru na wa haki.

Raila alidai- bila kutoa ushahidi- kwamba baadhi ya kaunti zimepata ongezeko lisiloelezeka la wapiga kura wao katika sajili.

Sajili hiyo inakaguliwa na KPMG na inatarajiwa kutangazwa katika gazeti la serikali siku zijazo mara itakapokabidhiwa kwa IEBC.

Miezi ya kabla na baada ya uchaguzi imekuwa nyakati za ghasia katika historia ya nchi hiyo baada ya uhuru.

Wengi wameuawa na mamia kuhama makazi yao wakati wa mzunguko wa uchaguzi tangu 2007.