Ngunjiri ataja sababu za wanasiasa wa Mt Kenya kutotumia picha za Raila kwenye mabango yao

Muhtasari

•Ngunjiri alieleza kuwa wagombea wanajaribu kujitofautisha na Raila kwa kuuza ajenda zao binafsi.

•Alisema wagombea hawakutaka kuchaguliwa kwa sababu ya Raila bali kwa sababu ya manifesto zao.

Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu akiwahutubia waandishi wa habari
Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu akiwahutubia waandishi wa habari
Image: MAKTABA

Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu amesema viongozi wa Mlima Kenya wanaoshirikiana na muungano wa Azimio la Umoja One Kenya hawatatumia picha za Raila Odinga kwenye mabango yao ya kampeni.

Alisema ni mkakati wa kisiasa ambao wagombe katika eneo lote la Mlima Kenya wanautumia kwani wanataka kuchaguliwa mwezi Agosti kwa kuzingatia manifesto zao na sio chama.

Akiwahutubia waandishi wa habari siku ya Alhamisi, Ngunjiri alieleza kuwa wagombea wanajaribu kujitofautisha na mgombea urasi wa Azimio-One Kenya kwa kuuza ajenda zao binafsi.

Ngunjiri alisema wagombea hawakutaka kuchaguliwa kwa sababu ya Raila bali kwa sababu ya manifesto zao.

"Tunataka watu wachaguliwe kwa kuzingatia msimamo wao binafsi ili tusichanganywe. Tunajaribu kuzalisha kipengele hicho cha uwajibikaji binafsi," alisema.

"Hatutaki kuwachanganya wapiga kura kwa kujificha nyuma ya watu fulani."

Wambugu pia alisema kuwa na kiongozi wa chama kwenye bango sio dhibitisho tosha kuonyesha uaminifu kwa chama.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa bado wanaeneza azma ya Raila kuwa rais, akiongeza kuwa mkakati wao unafanya kazi kwa manufaa yao.

Tunauza mgombea wetu wa urais lakini wakati huu, ikilinganishwa na 2017, kuna tofauti. Hii ni kwa sababu 2017, kulikuwa na watu ambao walichaguliwa kwa sababu ya Rais Uhuru Kenyatta lakini mara moja wakaingia afisini, wakaanza kumhujumu,” akasema.