Wajackoyah afunguka kuhusu familia yake

Muhtasari

•Wajackoyah amefichua kuwa watoto wake wanaishi Uingereza ilhali mkewe anaishi Marekani ambako ni nchi yake ya kuzaliwa.

•Alieleza kuwa tayari kuna mpango familia yake kuhamia humu nchini baada ya kupata uraia wa Kenya.

Mgombeaji wa urais wa chama cha Roots George Wajackoyah akiwasili katika eneo la BOMAS of Kenya kuwasilisha stakabadhi za kuania urais kwa IEBC
Mgombeaji wa urais wa chama cha Roots George Wajackoyah akiwasili katika eneo la BOMAS of Kenya kuwasilisha stakabadhi za kuania urais kwa IEBC
Image: EZEKIEL AMING'A

Mgombea urais kwa tikiti ya Roots Party of Kenya George Wajackoyah ameweka wazi  kuwa yeye ni mtu mwenye familia.

Akizungumza kwenye mahojiano katika Citizen TV, Wajackoyah alifichua kuwa ana mke na watoto ambao wanaishi nje ya Kenya.

Mgombea urais huyo alisema watoto wake wanaishi Uingereza ilhali mkewe anaishi Marekani ambako ni nchi yake ya kuzaliwa.

"Nina watoto na mke wa Marekani. Anaishi Marekani na watoto wetu watu wazima wanaishi Uingereza," alisema

Alieleza kuwa tayari kuna mpango familia yake kuhamia humu nchini baada ya kupata uraia wa Kenya.

Wajackoyah ni mgombea urais kwa mara ya kwanza ambaye amewasisimua Wakenya wengi hasa wenye umri wa ujana.

Mipango yake yenye utata kwa nchi hii na ucheshi wake umeingiza jina lake kinywani mwa mamilioni ya Wakenya ambao baadhi yao tayari wameahidi kumpigia kura.

Wajackoya tayari ameeleza kuwa iwapo atatwaa urais basi mradi wake wa wanza utakuwa kuhalalisha bangi kwa madhumuni ya dawa ili kupata mapato.

Mgombea urais huyo ameahidi kulipa madeni yote ya Kenya kwa mataifa mengine kutumia mapato ya bangi.

"Bangi itahalalishwa kwa mauzo ya nje ndio tulipe madeni ya China. Matumizi ya kujiburudisha yatakuwepo ingawa yatadhibitiwa. Gunia moja ya bangi huenda ikagharimu dola milioni 3.4. Nitalipa China madeni ya babaraba kwa takriban gunia hamsini za bangi" Wajackoyah aliwahi kusema katika mahojiano.

Kiongozi huyo wa Roots Party pia amepanga kuzindua ukulima wa nyoka iwapo atashinda kinyang'anyiro cha Agosti 9.

Kulingana naye, sumu ya nyoka ina thamani kubwa ambayo inaweza kuendesha uchumi wa nchi sambamba na kilimo cha bangi.

"Tunaanzisha ufugaji wa nyoka nchini ili tuweze kukamua sumu ya nyoka kwa madhumuni ya dawa, watu wengi wanaumwa na nyoka hapa nchini na inabidi msubiri dozi kutoka nje ya nchi kupitia shirikisho la dawa," Wajackoya alisema katika mahojiano na Citizen TV Jumatano jioni.

Wajackoyah alisema baada ya utoaji wa sumu nyoka hao watasafirishwa nje ya nchi kama chakula kwa nchi zinazokula nyama yake.

Hii, alisema, itazalisha mapato ambayo yanaweza kulipa deni kubwa la nchi.

"Tuna walaji nyoka wengi kama Wachina. Moja ya njia tunazoweza kulipa madeni ya Wachina ni kutoa sumu kutoka kwa nyoka na kuwapa Wachina nyama ya kula na kuwaambia ni malipo ya deni."

Wajackoyah ni mmoja wa wanne ambao IEBC ilipatia kibali cha kuwania kiti hicho cha juu zaidi kwenye uchaguzi wa Agosti 9, mwaka huu.