Ruto akejeliwa vikali kwa kunukuu mstari wa Bibilia ambao haupo

Muhtasari

• DP alinukuu mstari wa Biblia kueleza jinsi mitume wa Yesu walivyomwuliza mpango wake kwao baada ya kuacha kazi zao ili kumfuata.

•Kuteleza huko kwa naibu rais kumezua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii huku wapinzani wake wakiendelea kumkosoa. 

Image: FACEBOOK// WILLIAM RUTO

Naibu Rais William Ruto kwa mara nyingine amejipata kwenye utata baada ya kunukuu mstari wa Biblia ambao haupo. 

Katika mahojiano na NTV Jumapili jioni, DP alinukuu mstari wa Biblia kueleza jinsi mitume wa Yesu walivyomwuliza mpango wake kwao baada ya kuacha kazi zao ili kumfuata.

“Katika kitabu cha Mathayo 17:29, wanafunzi wa Yesu Kristo walipokuwa wakimfuata, walimwuliza, Sisi tumeziacha familia zetu, tumeacha biashara zetu. Tulikuwa wavuvi, tumekuja kukufuata, ni nini ulicho nacho  kwa ajili yetu?" Ruto alisema.

 Imebainika kuwa kifungu cha Biblia ambacho naibu rais alinukuu hakipo. Kitabu cha Mathayo 17 kinaishia kwenye mstari wa 27.

 Ujumbe ambao DP alinukuu unatoka kwenye Mathayo 19:27  ambayo inayosema: “Petro akamjibu, Sisi tumeacha kila kitu ili kukufuata wewe. Tutapata nini basi".

Kuteleza huko kwa naibu rais kumezua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii huku wapinzani wake wakiendelea kumkosoa. 

Ruto ambaye kwa kawaida hujitambulisha kama Mcha Mungu wa kweli, ameendelea kukejeliwa na baadhi ya Wakenya wakiwemo viongozi wanaounga mkono muungano wa Azimio- One Kenya. 

Akizungumzia kosa hilo, Gavana wa Kitui Charity Ngilu alisema: "Mathayo Sura ya 17 inaishia mstari wa 27. Msifuni Bwana". 

Gavana wa Nairobi Anne Kananu kwa upande wake aliuliza: "Mathayo 17:29? Ni mstari gani huo bosi? Haipo. Au tunatumia Biblia tofauti?"

Hizi hapa hisia za baadhi ya wanamitandao