Gachagua ni dikteta, nilimuonya Ruto asimteue kama mgombea mwenza- Kabogo

Muhtasari

•Gavana huyo wa zamani  alisema alimwambia Ruto kuwa mbunge huyo wa Mathira atamgharimu kura nyingi.

•Kabogo alimshutumu Ruto na chama cha UDA kwa kupanga kudhalilisha vyama shirika katika eneo la Mlima Kenya.

•Kabogo na Kuria  walitangaza kujiondoa kwenye kampeni za UDA kutokana na kutotendewa haki na vitisho kutoka kwa chama cha UDA.

WILLIAM KABOGO
Image: WILLIAM KABOGO/TWITTER

Aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo amedai kuwa alimuonya naibu rais William Ruto kutomchagua mbunge wa Mathira Rigathi Gachaguas kama mgombea mwenza wake.

Gavana huyo wa zamani ambaye anaonekana kutofautiana na Gachagua alisema alimwambia Ruto kuwa mbunge huyo wa Mathira atamgharimu kura nyingi.

Kabogo alisema hayo alipokuwa akiwahutubia wafuasi wake mjini Thika siku ya Alhamisi.

Alimcharukia Gachagua akimshutumu kuwa ndiye mpangaji mkuu wa masaibu yanayokumba vyama shirika katika Muungano wa Kenya Kwanza kutoka eneo la Mt Kenya.

"Kabla ya kuchaguliwa Rigathi Gachagua na William Ruto, mimi nilikua nimepinga," alisema.

Aliongeza "Amechaguliwa ndiyo maneno ya UDA na sisi imeanza kuzoroteka. Kwa sababu huyo jamaa ni dikteta. Makosa yangu nikusema kweli kwa sababu niliambia Ruto atapoteza kura nyingi kwa huyu jamaa."

Kabogo aliendelea kumshutumu Ruto na chama cha UDA kwa kupanga kudhalilisha vyama shirika katika eneo la Mlima Kenya.

Alidokeza kuchukua njia yake ya kisaisa mwenyewe baada ya kuwaambia wakazi wa Thika kuwa amekuja kupata baraka zao.

"Mimi nimerudi hapa kwa baba nataka kuanza safari mpya. Sipendi kwenda bila kufika nyumbani. Nimeona William Ruto na chama chake cha UDA wanataka kumeza vyama vyote. Na mimi nimekataa kumezwa."

Gavana huyo wa zamani pia alitilia shaka ustahiki wa Gachagua kuwa Naibu Rais.

Alipuuzilia mbali uwezekano wa yeye kumrithi DP Ruto kama Rais akisema yeye ndiye mfalme wa eneo la Mlima Kenya.

"Wewe piga hesabu, ati William Ruto ameshindwa na kazi ati Rigathi Gachagua atakua rais, Mimi ndo kiongozi wa wakaaji wa mlima Kenya. "

Haya yanajiri huku kukiwa na mzozo mkali uliosababishwa na madai ya upendeleo wa Gachagua kwa mgombea ugavana wa Kiambu kwa tiketi ya UDA Kimani Wamatangi.

Kabogo na kiongozi wa chama cha CCK Moses Kuria ambao pia wako kwenye kinyang'anyiro cha kuwania ugavana wa kaunti hiyo katika kambi ya Kenya Kwanza wametoa malalamishi kutokana na madai hayo.

Viongozi hao wawili wameelezea wazi kutoridhishwa kwao kuhusu namna UDA imekuwa ikiwashughulikia wao na vyama vingine vya kando kutoka eneo la Mlima Kenya.

Kabogo na Kuria siku ya Alhamisi walitangaza kujiondoa kwenye kampeni za UDA kutokana na kutotendewa haki na vitisho kutoka kwa chama cha UDA.