IEBC imeorodhesha wapiga kura wapya milioni 2.5,yaongeza vituo 6,000 vya kupigia kura

Muhtasari
  • Ripoti ya ukaguzi ya KPMG inaonyesha IEBC ilisajili wapigakura wapya milioni 2.5 waliosajiliwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita
MWENYEKITI WA IEBC WAFULA CHEBUKATI
Image: EZEKIEL AMING'A

Ripoti ya ukaguzi ya KPMG inaonyesha IEBC ilisajili wapigakura wapya milioni 2.5 waliosajiliwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Akitoa matokeo hayo Jumatatu, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema ripoti hiyo inaonyesha idadi ya waliosajiliwa ilipanda kutoka 19,611,423 mwaka wa 2017 hadi 22,120,458 mwaka wa 2022.

Chebukati pia alisema kumekuwa na ongezeko la asilimia 13.08 la vituo vya kupigia kura kati ya chaguzi kuu mbili.

"Mwaka wa 2017 tulikuwa na vituo 40,883 vya kupigia kura, kwa 2022 tuna vituo 46,232," Chebukati alisema.

Bosi huyo wa shirika la uchaguzi alisema pia kumekuwa na ongezeko la milioni 2.6 la idadi ya wapiga kura wanaostahiki nchini katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Alisema takwimu kutoka Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya (KNBS) zinaonyesha kuwa mwaka wa 2017, kulikuwa na wapigakura 25,212,096 waliotimiza masharti ya kupiga kura ikilinganishwa na 27,857,598 mwaka wa 2022.

Alisema takwimu za Ofisi ya Taifa ya Usajili (NRB) pia zinaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la vitambulisho vya taifa vilivyotolewa tangu mwaka 2017.

Mnamo 2017, alisema, NRB ilitoa vitambulisho 25,323,059 ikilinganishwa na vitambulisho 29,566,678 vilivyotolewa mwaka wa 2022.

Hii, alisema, inawakilisha ukuaji wa asilimia 16.76.

"Ukiangalia kiwango cha uandikishaji, mwaka wa 2017 waliosajiliwa wapiga kura na IEBC ikilinganishwa na waliohitimu na KNBS waliwakilisha asilimia 77.78 na 2022 inawakilisha asilimia 79.41," Chebukati alisema.

Alisema wapigakura waliosajiliwa na IEBC mwaka wa 2017 ikilinganishwa na idadi ya vitambulisho vilivyotolewa na NRB mwaka wa 2017 ni asilimia 77.44.

Mnamo 2022, kiasi kilipungua hadi asilimia 74.82.

Alisema pia kumekuwa na ongezeko kubwa la wapiga kura waliojiandikisha kwenye diaspora na magereza.

Chebukati alisema idadi ya waliojiandikisha kupiga kura katika mataifa ya ughaibuni mwaka wa 2017 ilikuwa 4,223 ikilinganishwa na 10,444 mwaka wa 2022.

Wafungwa waliosajiliwa mnamo 2017 walisimama kwa 5,182 ikilinganishwa na 7,483 mnamo 2022.