Kura ya maoni:Sifuna ndiye mgombea useneta maarufu Nairobi

Muhtasari
  • Data ya utafiti ilikusanywa kupitia mbinu ya simu tarehe 20 Juni
  • Jumla ya wahojiwa 632 (wapigakura waliojiandikisha) kutoka maeneo bunge yote 17 walihojiwa
Image: Manuel Odeny

Katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna angeshinda kinyang'anyiro cha useneta wa Nairobi ikiwa uchaguzi ungefanyika leo, kura ya maoni ya Tifa Utafiti unaonyesha.

Utafiti huo ulisema Sifuna alikuwa na kiwango cha kuidhinishwa cha asilimia 27 ikilinganishwa na mpinzani wake wa karibu, Askofu wa UDA Margaret Wanjiru, aliyepata asilimia tisa.

"Hata hivyo kwa kuwa karibu theluthi mbili ya wakazi wa Nairobi hawajaamua kuhusu kinyang'anyiro hiki (au kuwa tayari kumpigia mtu yeyote kura kabisa) asilimia 64, ni mapema mno kujua matokeo yatakuwaje," utafiti ulisema.

Kura ya maoni ilibainisha kuwa kiwango cha kuidhinishwa na Sifuna kilipanda kutoka asilimia 19 hadi asilimia 27 mwezi Juni huku kile cha Wanjiru kilipanda kutoka asilimia sita hadi tisa katika kipindi hicho.

Mbunge mteule Maina Kamanda alikuwa na ukadiriaji wa kuidhinishwa wa asilimia moja mwezi wa Mei, ambao ulishuka hadi sifuri mnamo Juni. Mnamo Mei, asilimia 73 ya waliohojiwa hawakuwa wameamuliwa lakini idadi ilipungua kwa asilimia tisa hadi 64 mwezi Juni.

Data ya utafiti ilikusanywa kupitia mbinu ya simu tarehe 20 Juni

Jumla ya wahojiwa 632 (wapigakura waliojiandikisha) kutoka maeneo bunge yote 17 walihojiwa.

Upeo wa makosa ya utafiti ulikuwa kuongeza au kutoa 3.8%.