Wajackoyah atoa onyo kali kwa kanisa baada ya kupinga uhalalishaji wa bangi

Muhtasari

•Wajackoyah alishutumu kanisa kwa unafiki na kuonya kuwa huenda vijana wakaanza kuzisusia hivi karibuni.

•Mgombea urais huyo Aidha alisema ni jukumu la viongozi wa kidini kuwaombea watenda dhambi ila sio kuwahukumu.

Mgombeaji wa urais wa chama cha Roots George Wajackoyah akiwasili katika eneo la BOMAS of Kenya kuwasilisha stakabadhi za kuania urais kwa IEBC
Mgombeaji wa urais wa chama cha Roots George Wajackoyah akiwasili katika eneo la BOMAS of Kenya kuwasilisha stakabadhi za kuania urais kwa IEBC
Image: EZEKIEL AMING'A

Mgombea urais George Wajackoyah ametoa onyo kali kwa viongozi wa kanisa kwa kupinga wazo  lake ya kuhalalisha bangi.

Akizungumza Jumatatu, Wajackoyah alishutumu kanisa kwa unafiki na kuonya kuwa huenda vijana wakaanza kuzisusia hivi karibuni.

"Ni wakati wa wao pia kugundua kuwa Kenya sio yao. Wengine wetu tumelelewa Kikristo. Waambiwe wafanye mikakati ya kutafutia watu kazi. Kuna pesa ya wizi ambayo wamekuwa wakichukua kila siku wanakula," Wajackoyah alisema.

Kiongozi huyo wa Roots Party pia aliwashtumu baadhi ya maaskofu kwa uasherati na wizi huku akibainisha kuwa wao ndio wanafaa kuhukumiwa.

Aidha aliongeza kuwa ni jukumu la viongozi wa kidini kuwaombea watenda dhambi ila sio kuwahukumu.

"Acha kanisa lijue kwamba lina wajibu wake wenyewe kuwaombea watu kama mimi. Ikiwa mimi ni mwendawazimu basi waniombee niwe na akili timamu. Hawana haki ya kunifundisha  kuhusu mahitaji ya Wakenya," Alisema.

Jumapili maaskofu wa Kikatoliki walivunja ukimya wao kuhusu kampeni za kisiasa zinazoendelea na kuwataka wapiga kura kukataa mapendekezo yasiyo ya kawaida ya wagombea. 

Katika shambulio fiche kwa Wajackoyah, Baraza la Maaskofu wa Kikatoliki nchini Kenya lilisema Wakenya hawafai kuwapigia kura wanasiasa wanaopendekeza sera zinazolenga kuhalalisha matumizi ya dawa za kulevya.

Askofu Mkuu wa Nyeri Anthony Muheria ambaye alizungumza kwa niaba ya makasisi hao pia aliwataka wapiga kura kuwakataa viongozi wanaounga mkono uavyaji mimba na wale walio na ajenda ya kuhalalisha tabia zilizoharamishwa za ngono zikiwemo ponografia.

Viongozi hao wa kidini pia wanataka wapiga kura kuwakataa viongozi wafisadi. Muheria aliwashauri wapiga kura kutafuta viongozi wanaojitolea kupigana na maovu na wanaotoa hatua madhubuti za jinsi ya kufanya hivyo.

“Tunawaomba mkatae kumchagua kiongozi yeyote ambaye tunaona ataeneza saratani ya ufisadi. Kiongozi anayechaguliwa anapaswa kuchukia rushwa katika ngazi zote na awe mfano kwa wengine,” alisema.

Muheria alisema kuwa ni lazima kiongozi awe mtu anayeheshimu sheria za Mungu na ambaye ataendeleza maadili ya kitamaduni ya Kiafrika na ya Kikristo.