Kabogo amkana Ruto, asema yuko kivyake

Muhtasari

• Swintofahamu ilianza wakati Kabogo na Moses Kuria walisusia mkutano wa kampeni ulioitishwa na DP katika eneo la Ndumberi, Kaunti ya Kiambu. 

 

William Ruto
William Ruto

Mgombea ugavana wa Kiambu William Kabogo amekana hadharani kuwa hana uhusiano wowote na Muungano wa Kenya Kwanza. 

Akizungumza wakati wa mdahalo wa wanaowania ugavana katika kaunti ya Kiambu kwenye Citizen TV, Jumapili, alisisitiza kuwa yeye si wa muungano huo ambao mgombeaji urais ni William Ruto, na kwamba yuko peke yake. 

"Mambo yanabadilika na kwa sasa niko peke yangu na ninaendelea vizuri," Kabogo alisema. 

Katika muda wa wiki tatu zilizopita, mgogoro kati ya Kabogo na naibu rais William Ruto umejitokeza hadharani na kumlazimu gavana huyo wa zamani wa Kiambu kufanya kampeni zake peke yake. 

Swintofahamu ilianza wakati pamoja na kiongozi wa Chama Cha Kazi Moses Kuria walisusia mkutano wa kampeni ulioitishwa na DP katika eneo la Ndumberi, Kaunti ya Kiambu, wiki mbili zilizopita. 

Wawili hao walipinga kudhalilishwa na chama cha UDA ambacho walisema kilikuwa kinamfanyia kampeni mgombeaji wake Kimani wa Matangi pekee ilhali muungano wa Kenya Kwanza ulikuwa na wagombeaji wengine wa ugavana. 

Kabogo na Kuria walitoa wito wa kuwepo kwa mazingira sawa huku kila muaniaji akitafuta kura kuongoza kaunti ya Kiambu. Kuria ambaye kwa sasa amesuluhisha tofauti zake na Ruto ameanza kuhudhuria mikutano ya Kenya Kwanza.

Kabogo kwa upande wake emejiweka mbali. Alishutumu chama cha United Democratic Alliance kinachoongozwa na Ruto kwa kumfungia nje linapokuja suala la kupanga mikutano katika eneo la Mlima Kenya. 

Kabogo alionya zaidi timu ya Kenya Kwanza kuwa makini na mkakati wao wa kampeni katika eneo hilo, akisema kuwa uteuzi wa mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua kama mgombea mwenza kumefanikisha umaarufu wao katika eneo hilo.