Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi 'arejea shuleni'

Muhtasari

• Mitandao ya kijamii imewaka baada ya picha za Oscar Sudi kuvujishwa akiwa katika sare ya shule.

• Wengi walizua utani kutokana na kesi inayomkabili mbunge huyo baada ya chuo anuwai na shule ya upili kukataa kwamba hakuhudhuria masomo.

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi
Image: Raila na Karua (Facebook)

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi amezua gumzo mitandaoni baada ya kuonekana akiwa kwenye sare za shule pamoja na wanafunzi wengine.

Uchunguzi wa kina ulionesha kwamba mbunge huyo alivaa sare hiyo ya shule ya upili ya Simat ili kuhudhuria hafla iliyokuwa ikifanyika shuleni humo.

Wakenya mbalimbali walijitokeza kuzua utani mkali wa kufurahisha na wa kuchukizwa kwa viwango sawa kuhusu mbunge huyo ambayemwaka jana aligonga vichwa vya habari baada ya mahakama kudai kwamba vyeti vyake vya shule ya upili na chuo anuwai ni bandia.

Kesi hiyo iliyopelekwa mahakamani baada ya tume ya kusimamia uchaguzi IEBC kupata kwamba vyeti vyake vilikuwa ghushi wakati alikuwa anataka kuruhusiwa kugombea ubunge mnamo mwaka 2013.

Masaibu ya Sudi yalizidi kuongezeka baada ya madai kuibuka kwamba aliyekuwa mwalimu mkuu wa shule ya upili ambapo Sudi alidai kuhudhuria masomo yake ya sekondari kukana kwamba Sudi hakuwa mwanafunzi wake.

Jungu la matatizo yanayozingira elimu ya mbunge huyo lilizidi kutokota hata zaidi baada ya chuo anuwai cha Kenya Institute of Management Studies kukataa mwaka jana kwamba Sudi alipata diploma yake katika masuala ya biashara kutoka chuo hicho.

Baada ya picha hiyo kuvujishwa mitandaoni, utani umezidi huku baadhi sasa wakisema hatimaye mbunge huyo amerudi shule ya upili kumaliza masomo yake.

Baadhi walimlimbikizia mwanablogu Robert Alai sifa kochokocho kwa kuwa katika mstari wa mbele kutumbua wale ambao wameshikilia nyadhifa mbalimbali za kisiasa pasi na sitakabadhi halisi huku wengine wakimtaka mbunge wa Embakasi mashariki Babu Owino kuwarudisha darasani na kuwapa mafunzo.

“Robert Alai asante kwa kusafisha uongozi wa nchi hii kuhusu sifa za kitaaluma. Oscar Kipchumba Sudi ameamua kurejea darasani tu. Mhadhiri wetu Babu Owino atampokea kwa ajili ya kusajiliwa,” aliandika mtumizi mmoja wa mtandao wa Facebook.

Ikumbukwe mwanablogu Alai amekuwa katika mstari wa mbele kuwakosoa na kuanika masomo ya baadhi ya viongozi wanaotajwa kughushi vyeti vya masomo ili tu kupata nafasi ya kuwania nyadhifa za uongozi.

Baadhi ya wanasiasa ambao Alai ametumbua utata wav yeti vyao ni pamoja na maseneta Johnson Sakaja na Cleophas Malala na mbunge wa Malindi Aisha Jumwa ambo kulingana na Alai vyeti vyao ni vya kutiliwa mashaka.