Raila aahidi kukabili mauaji ya kiholela na kuboresha idara ya mahakama

Muhtasari

• viongozi waliwarai wenyeji kuwapigia kura kwenye uchaguzi mkuu ujao wakiahidi kuleta mabadiliko na uongozi bora nchini.  

Mgombea urais wa Azimio one Kenya Alliance Raila Odinga akiwahutubia wananchi eneo ka Daadab, 27/6/2022.
Mgombea urais wa Azimio one Kenya Alliance Raila Odinga akiwahutubia wananchi eneo ka Daadab, 27/6/2022.
Image: Azimio Media

Idara ya mahakama nchini itaangaziwa upya katika juhudi za kuhakikisha visa vya mauwaji ya kiholela na vijana kutoweka kwa njia tatanishi vinazikwa katika kaburi la sahau, viongozi wa muungano Azimio La Umoja – OKA wamesema.

Wakihutubia mikutano ya hadhara katika kaunti ya Garissa siku ya Jumatatu, viongozi wa muungano huo wakiongozwa na kinara wao Raila Odinga waliwarai wenyeji kuwapigia kura kwenye uchaguzi mkuu ujao wakiahidi kuleta mabadiliko na uongozi bora nchini.  

Mgombea mwenza wa Raila Martha Karua kwa upande wake alisema jukumu lake kuu litakua kuhakikisha anatumia mamlaka, tajriba na weledi wake kufanikisha vita dhidi ya ufisadi.

Image: Azimio Media

Karua alisisitiza umuhimu wa vita dhidi ya ulaji rushwa akisema kwamba umechangia sana masaibu wanayopitia wakenya.

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth ambaye pia alikuwa ameandamana na Raila aliwasuta viongozi wa muungano wa Kenya Kwanza kwa kutumia visivyo swala la kupanda kwa gharama ya maisha kujipigia debe, akisema chanzo cha kupanda kwa gharama ya maisha ni mswaada uliofadhiliwa na mbunge wa chama cha UDA Aden Duale.

Wakati huo huo Katibu wa muungano wa wafanyikazi nchini (Cotu) Francis Atwoli, wabunge Babu Owino (Embakazi mashariki), Dkt. Makali Muli (Kitui ya kati) na Stephen Mule (Matungulu) nao walimkosoa naibu wa rais William Ruto wakisema kwamba ni kiongozi asiyekuwa na sera madhubuti.

Image: Azimio Media

Walimshtumu Ruto kwa kujaribu kujinasua kutoka kwa makosa ya serikali ya Jubilee na kujipendekeza tu kwa mazuri ya serikali hiyo.