(Video)"Sifuna Utaanguka tena, achana na Mathare na ufagie kwako" - Bahati

Muhtasari

• Msanii Bahati amempa mzomo katibu mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna ambaye alimtaka kutupilia mbali azma yake ya kuwa mbunge wa Mathare na kumuunga mkono mpinzani wake, Oluoch.

Kelvin Bahati Kioko anayelenga ubunge Mathare kupitia chama cha Jubilee
Msanii Bahati Kelvin Bahati Kioko anayelenga ubunge Mathare kupitia chama cha Jubilee
Image: Instagram screenshot

Mwanamuziki Kevin Kioko almaarufu Bahati ambaye pia analenga kiti cha ubunge Mathare kupitia tikiti ya Jubilee amemkosoa vikali katibu mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna kwa matamshi yake kwamba vuguvugu la Azimio lacUmoja limeamua kumuunga mkono Anthony Oluoch wa ODM katika kinyang’anyiro cha ubunge Mathare.

Juzi katika mkutano mkuu wa muungano wa Azimio la Umoja, kulisemekana kuwa na maelewana ya kushawishi baadhi ya wawaniaji wa vyama vingine ndani ya muungano huo kutupilia mbali azma yao ya kugombea na badala yake kuwaunga mkono wawaniaji wenza ambao wanaonekana kuwa na ushawishi mkubwa katika kuzoa kura, ili kuhakikisha kwamba muungano huo unapata uwakilishi mkubwa katika nyadhifa mbalimbali.

Kufuatia maelewano hayo, Sifuna alimtaka Bahati wa Jubilee kutupilia mbali azma yake ya kuwa mbunge wa Mathare na badala yake kumuunga mkono mbunge wa sasa Anthony Oluoch ambaye analenga kukitetea kiti hicho kwa tikiti ya chama cha ODM.

Bahati ambaye alichukizwa na matakwa hayo ya katibu mkuu wa ODM aliamua kukunja shati na kujibwaga ulingoni katika kutupiana maneno makali na Sifuna huku akimtaka aachane na eneo bunge la Mathare kabisa kama kweli anataka kura za eneo bunge hilo kumvusha kuwa Seneta wa Nairobi.

“Mimi nashangaa na huyu Sifuna, 2013 alikuwa na tikiti ya ODM huko Kanduyi na akaanguka, 2017 alikuwa na tikiti ya ODM na bado akaanguka Seneta hapa Nairobi. Na huyu jamaa vile anaendelea kuchezea youth, hana heshima kwa youth, hata huu mwaka tutakuwa tulifanya maamuzi mabaya kama Azimio, ataanguka tena! Sifuna fagia kwako,” Bahati anaonekana akifoka katika mkanda wa video uliosambazwa mitandaoni Jumatatu.