Ruto: Kenya Kwanza itaunga mkono mfumo wa kielektroniki wa kutambua wapiga kura

Muhtasari

• Ruto alisema vuguvugu la Kenya Kwanza litaunga mkono mfumo wa kielektroniki na kuitaka IEBC kuhakikisha wapiga kura wote wanajumuishwa

Kinara wa Kenya Kwanza, William Ruto
Image: William Samoei Ruto (Facebook)

Naibu wa rais William Ruto ambaye analenga kuwa rais wa tano katika uchaguzi wa Agosti 9 sasa amesema kwamba muungano wa Kenya Kwanza anaouongoza umeafikiana na IEBC na kukubali kuunga mkono takwa la tume hiyo ya kuratibu na kuandaa uchaguzi kwamba itatumia mfumo wa kielektroniki wa kuwatambua wapiga kura.

Akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook Jumatano alasiri pindi tu baada ya kuhudhuria mkutano wa wagombea urais ulioitishwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, Ruto alisema kwamba vuguvugu la Kenya Kwanza litaunga mkono kikamilifu IEBC kutumia mfumo huo wa kidijitali kuwatambua wapiga kura wote.

Aidha, Ruto aliitaka tume hiyo kuhakikisha kwamba katika matumizi ya kielektroniki, wapiga kura wote wapate kutambuliwa na kuruhusiwa kupiga kura kwani ni haki yao ya kidemokrasia na kusema kwamba mpiga kura yeyote asikose kupiga kura kwa kukosa kutambuliwa na mfumo huo wa kielektroniki.

“Kenya Kwanza inaunga mkono matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa kutambua wapiga kura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9. Tunatoa wito kwa tume ya uchaguzi kuhakikisha sajili hiyo inajumuisha wapiga kura wote. Nilihudhuria mkutano wa mashauriano wa Tume Huru za Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na wagombeaji Urais katika Hoteli ya Windsor Golf, Kaunti ya Jiji la Nairobi,” Ruto aliandika.

Awali picha za Ruto akiwa anasalimiana kwa mkono na mpinzani wake wa karibu ambaye pia ni kinara wa muungano wa Azimio-One Kenya, Raila Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua zilihanikiza kwenye janibu za mitandao ya kijamii huku baadhi wakizitumia kuelezea falsafa ya siasa kwamba wanasiasa hawana uadui bali tu kila mmoja anapigania matakwa yake na wao ni marafiki wakubwa.

Wengi wa Wakenya walisema kwamba viongozi wote ni marafiki na hawana tofauti zozote kisiasa kama wanavyoigiza katika umma na hivyo kuwataka ndugu zao wasikubali kugawanyishwa kwa misingi ya marengo ya kisiasa wakati huu ambapo taifa linajiandaa kuelekea uchaguzi mkuu takribani siku arobaini hivi.

Picha za wawili hao wakisalimiana kwa tabasamu kubwa zilichukuliwa na wanahabari pindi tu baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa mashauriano ulioitwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati.