Nitamlinda waziri Matiang'i-Raila asema huku akiwakashifu wapinzani wake

Muhtasari
  • Akizungumza katika ziara ya kampeni huko Nyamira siku ya Ijumaa, Odinga alimsifu Matiang’i kama kiongozi mkuu akisema atamlinda dhidi ya mashambulizi yoyote ya kisiasa
Kinara wa ODM Raila Odinga
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Mgombea urais wa Azimio La Umoja One Kenya  Raila Odinga amemtetea Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt. Fred Matiang’i kuhusu mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa viongozi washirika wa muungano wa Kenya Kwanza.

Akizungumza katika ziara ya kampeni huko Nyamira siku ya Ijumaa, Odinga alimsifu Matiang’i kama kiongozi mkuu akisema atamlinda dhidi ya mashambulizi yoyote ya kisiasa.

Waziri Mkuu huyo wa zamani aliwaambia wakazi kwamba Waziri huyo alikuwa akikosolewa kwa ujasiri wake katika kutumikia nchi. Odinga aliihakikishia jamii ya Wakisii anakotoka Matiang’i kwamba angemtia ndani ya serikali yake iwapo atapanda mamlaka katika uchaguzi ujao.

“Fred Matiang'i tumetoka mbali na amefanya kazi nzuri. Tumefanya naye kazi kwa muda mrefu lakini sasa anapingwa na wale watu wengine unaowajua… Wanamshambulia lakini yuko chini ya ngao ya Baba,” Odinga alisema.

“Nitamlinda. Hapa chini, ninawaona nyinyi (wapiga kura) mmesimama imara pamoja na Matiang’i… na pale juu nitakuwa nimesimama naye. Tutaendelea kufanya kazi naye baada ya tarehe 9 Agosti."

Waziri Mkuu huyo wa zamani vile vile aliwashutumu wapinzani wake kwa kuandamana dhidi ya Mataing’i kwa vile alikuwa akipinga madai yao maovu.

“Ni mtu anayejua kufanya kazi zake na ndiyo maana wahalifu wanapambana naye; wale wakora wanampiga kwa sababu ya ile kazi nzuri ambayo anaifanya,” Odinga alisema.

Kuhusiana na mzozo unaoendelea katika kaunti za Kisii na Migori kuhusu siasa za vyama vinavyohusishwa na Azimio, Odinga aliwataka wapiga kura kufanya chaguo lao kwa kuwapigia kura viongozi maarufu ndani ya Azimio.