"Hata Trump alitishia kupiga mtu risasi na bado akapigiwa kura!" Seneta Kang'ata amtetea Ruto

Irungu Kang'ata alimtetea naibu rais William Ruto dhidi ya madai ya kutaka kumpiga rais Kenyatta kofi

Muhtasari

• Kang'ata alisema madai hayo ya Ruto kutaka kumpiga Kenyatta kofi hayawezi kuwafanya wasimuunge mkono.

Seneta wa Murang'a Irungu Kang'ata katika kampeni
Irungu Kang'ata Seneta wa Murang'a Irungu Kang'ata katika kampeni
Image: Twitter

Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata amekuwa mtu wa hivi punde kujitosa mzima mzima katika Sakata linalomhusisha naibu rais William Ruto kutaka kumzaba kofi rais Uhuru Kenyatta mnamo mwaka 2017 rais alipoonekana kuvuta nyuma kushirika uchaguzi wa marudio ya uchaguzi huo.

Madai ya Ruto kutaka kumzaba kofi moja la moto rais Uhuru Kenyatta yaliibuliwa na mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed aliyecheza sauti ya Ruto akizungumza kwamba alitaka kumpiga kofi rais Kenyatta.

Suala hilo la Ruto kumzaba rais Kenyatta kofi lilitanda katika mitandao ya kijamii wikendi iliyopita ambapo viongozi walionekana kugawanyika katika marengo miwili, baadhi wakimtetea Ruto na wengine wakimkashfu kwa kitendo hicho alitaka kukifanya kwa rais Kenyatta.

Akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, seneta Kang’ata amemtetea Ruto akisema kwamba hata aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump alitishia kuwafyatulia risasi watu katika mtaa mmoja nchini Marekani lakini bado wakampigia kura.

Kulingana na Kang’ata, madai ya Ruto kutaka kumzaba kofi rais Kenyatta hayatawafanya kutompigia kura naibu rais.

“Donald Trump aliwahi kusema kuwa anaweza kumpiga risasi mtu mmoja kwenye mtaa wa Manhattan na bado akapata kura kutoka kwa wafuasi wake. Hakuna chochote WSR anaweza kusema au kufanya ili kupoteza uungwaji mkono wetu,” aliandika kang’ata.

Seneta huyo ambaye analenga kuwa gavana wa kaunti ya Murang’a kupitia tikiti ya chama cha UDA alizidi kumtetea Ruto zaidi huku akisema kwamba hata biblia yenyewe inasema kofi la Rafiki linaweza kuaminika kulinganishwa na busu la adui.

Alinukuu Biblia katika kitabu cha Methali 27 mstari wake wa sita na saba ambapo maandiko yanasema kwamba “Kofi la Rafiki linaweza kuaminika kusaidia kuliko nusu la adui ambalo halina chochote zaidi ya uongo mtupu.”

Akionekana kumchimba mikwara rais Kenyatta kwa kutetea manifesto ya muungano wa Kenya Kwanza kuhusu kupatia walala hoi kipaumbele, Kang’ata aliendelea kunukuu biblia katika kifungo hicho ambapo maandika katika mstari wake was aba yanasema kwamba “Ukiwa na shibe hata asali haina ladha kwako lakini ukiwa na njaa hata kitu chochote chenye uchachu kwako kitaonja ladha tamu.”