Tuwache kuwapotosha Wakenya!Chebukati ajibu madai ya wizi wa kura

Chebukati alisisitiza kuwa karatasi za kura zinachapishwa kulingana na idadi ya wapiga kura.

Muhtasari

•Wafula Chebukati alisisitiza kuwa karatasi za kura zinachapishwa kulingana na idadi ya wapiga kura.

•Chebukati alitoa hakikisho kuwa karatasi zote zitawasili kupitia JKIA na hakuna ambazo zitapitishiwa Uganda.

MWENYEKITI WA IEBC WAFULA CHEBUKATI
Image: EZEKIEL AMING'A

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amepuuzilia mbali madai kwamba kuna mpango wa kuchapishwa kwa karatasi zaidi za kupigia kura.

Akizungumza Alhamisi, Chebukati aliwasihi wanasiasa kutowapotosha Wakenya kuwa kuna mpango wa wizi wa kura.

Msimamizi huyo mkuu wa uchaguzi alisisitiza kuwa karatasi za kura zinachapishwa kulingana na idadi ya wapiga kura.

"Karatasi zote za kura zimewekwa nambari maalum na zinachapishwa karatasi 22, 120, 258 ambayo ni idadi ya wapiga kura kwa wadhifa wowote unaowaniwa.. Hakuna karatasi za ziada.," Chebukati alisema.

Chebukati alisema kuwa mnamo Agosti 9 kila kituo cha kupigia kura hapa nchini kitapokea karatasi zitakazowatosha  wapiga kura wake.

Aidha alifichua kuwa shehena ya kwanza ya karatasi za kura iko tayari na inatarajiwa kuwasili nchini leo. Alitoa hakikisho kuwa karatasi zote zitawasili kupitia uwanja wa ndege wa JKIA na hakuna ambazo zitapitishiwa Uganda.

"Tunapokea shehena ya kwanza ya karatasi za kura, zinafika nchini leo kupitia uwanja wa ndege. Karatasi zote zitapitia JKIA. Hakuna karatasi za kura kutoka Uganda ama mahali kwingine. Msikubali watu wawadanganye," Alisema.

Chebukati pia aliwahakikishia Wakenya kuwa tume imejiandaa vilivyo kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

"IEBC imejitayarisha kwa uchaguzi huu zaidi ya hapo awali. Tutahakikisha kwamba tuna mchakato wa uwazi, tutawapa Wakenya uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika. Hiyo ndiyo ahadi yetu kwa nchi," Alisema.

Alisema kuwa IEBC ni taasisi huru na hawatakubali taasisi zingine kuingilia kati kwa michakato ya uchaguzi.