Asilimia 70 ya wakazi wa Nairobi wanashindwa kuoga - Sakaja

Sakaja amedai kuwa wakazi wa Nairobi wanashindwa kuoga kwa kukosa maji.

Muhtasari

•Sakaja alisema kuwa changamoto kubwa inayokabili jiji la Nairobi ni suala la usambazaji ya maji.

•Sakaja pia alibainisha kuwa wakazi wa Nairobi wanahitaji lita milioni 850 za maji lakini wanapata lita milioni 525.6 za maji.

Johnson Sakaja, akihutubia wanahabari
Johnson Sakaja, akihutubia wanahabari
Image: RADIO JAMBO

Seneta wa Nairobi na ambaye anawania ugavana wa kaunti hiyo kwa tiketi ya United Democratic Alliance (UDA) Johnson Sakaja amedai kuwa asilimia 70 ya wakazi wa Nairobi wanashindwa kuoga kwa kukosa maji.

Akizungumza Jumatatu wakati wa Mdahalo wa ugavana Nairobi, Sakaja alisema kuwa changamoto kuu inayokabili mji mkuu ni suala la usambazaji ya maji.

"Lazima tusuluhishe suala la usambazaji kwa sababu maji yanakwenda sambamba na makazi'' Sakaja alisema.

"Nairobi inapata maji kutoka  kwa chemchemi za Kikuyu ambayo ilizinduliwa mwaka 1907 na kutoa asilimia moja. Baada ya hapo tukatengeneza bwawa la Tururu ambalo hutoa asilimia nne, la tatu ni Sasumwa ambalo hutoa asilimia 11 na la nne ni Bwawa la Ndakaini ambalo hutoa asilimia 84 ya maji yanayotumika Nairobi'' Sakaja alisema.

Sakaja pia alibainisha kuwa wakazi wa Nairobi wanahitaji lita milioni 850 za maji lakini wanapata lita milioni 525.6 za maji.

''Tunahitaji kuziba pengo hilo. Utashangaa kwamba asilimia 70 ya wakazi wa Nairobi hawajawahi kuoga," Sakaja aliongeza.

Sakaja atachuana na wagombeaji wengine saba wanaokimezaea mate kiti cha ugavana wa Nairobi katika uchaguzi wa Agosti 9.

Wote ni pamoja na Kenneth Nyamwamu (UPA), wagombea huru Esther Thairu na Agnes Kagure, Denis Kodhe (LDP), Nancy Mwadime (Usawa Kwa Wote) na Safina’s Herman Grewal.