"Katika tukio lisilo la kawaida kwamba nimeshindwa ugavana, nitaondoka siasani" - Moses Kuria

Alisema kwamba iwapo atashindwa basi siasa itakuwa mwisho wake.

Muhtasari

• " Si ukweli kabisa kwamba nimetuma jina langu kuteuliwa kama mbunge" - Kuria

• "Kuna maisha mengine tena zaidi ya haya ya siasa,” Kuria aliweka wazi.

Kinara wa Chama Cha Moses Kuria
Kinara wa Chama Cha Moses Kuria
Image: Facebook

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria sasa amejitokeza mazima kupuuzilia mbali madai ambayo ameyataja kama propaganda yaliyomhusisha na kujiteua kaam mbunge mteule bungeni.

Wikendi iliyopita, baada ya muungano wa kenya Kwanza kuweka wazi majina ya wanasiasa watakaoteuliwa kwenye bunge baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa Agosti, madai yaliibuka kwamba mbunge huyo ambaye anawania ugavana Kiambu amelituma jina lake kuteuliwa pia kama mbunge mteule.

Kuria sasa amepinga propaganda hizo na kusema kwamba sheria ipo wazi kabisa kwamba iwapo mtu anagombea kiti cha siasa basi hakuna vile anaweza tena kujiteua katika bunge lolote.

“Sheria ipo wazi kabisa, kama unagombea nafasi ya kisiasa hakuna vile unaweza ukalituma jina lako ili kuteuliwa katika orodha ya chama cha kisiasa. Si ukweli kabisa kwamba nimetuma jina langu kuteuliwa kama mbunge, akili zangu na fikira zangu zote ziko kwa kuchaguliwa kama gavana wa Kiambu na William Ruto kuchaguliwa kama rais wa nchi,” aliandika Kuria kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Mbunge huyo ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa rais Kenyatta tangu waungane na Raila Odinga alisema kwamba ana Imani matokeo hayo mawili yatafanikiwa na kusema kwamab kilichosalia ni kuwekwa rasmi tu baada ya Agosti 9.

Pia alisema kwamab ikitokea hajachagulia, tukio ambalo hana uhakika kama litatokea, basi hamtamuona katika siasa kabisa, ukiachia mbala hata huko kuteuliwa kunakosemekana.

“Katika tukio ambalo si la kawaida kwamba nimebwagwa katika uchaguzi, basi hamtaniona kabisa katika siasa, achia mbali kuteuliwa mnakong’aka. Kuna maisha mengine tena zaidi ya haya ya siasa,” Kuria aliweka wazi.