Moses Kuria amtaka Justina Wamae kujiondoa kuwa mgombea mwenza wa Wajackoyah

Alisema Wajackoyah ni mradi wa serikali

Muhtasari

“Sasa rafiki yangu Wangui kuwa na ujasiri kiasi na uache tikiti hiyo. Kama kaka yako nipo nyuma yako kwa hili," - Kuria kwa Wamae

Mgombea mwenza wa George Wajackoyah na mbunge wa Gatundu Kusini
Mgombea mwenza wa George Wajackoyah na mbunge wa Gatundu Kusini
Image: Facebook

Kinara wa Chama Cha Kazi ambaye pia ni mgombea ugavana katika kaunti ya Kiambu, Moses Kuria amemtaka mgombea mwenza wa George Wajackoyah, Justina Wamae kukitoa katika nafasi hiyo akidai anajua fika kwamab Wajackoyah ni mradi wa Raila.

Kupitia ujumbe huo ambao Kuria aliutuma kwa Wamae kwenye ukurasa wake wa Facebook Jumanne asubuhi, Kuria anadai kwamab Justina Wamae anajua vizuri sana kwamba kinara wa chama chao cha Roots ni mradi wa Raila ambao umeundwa ili kuvuruga kura na kulazimisha marudio ya kura za urais.

“Kwa rafiki yangu mzuri Justina Wangui Wamae. Unajua ukweli usiogope kuchukua hatua. Unajua rafiki yetu George Luchiri Wajackoyah ni mradi wa serikali wa kumuunga mkono Raila Odinga, kulazimisha marudio ya urais na kuongeza muhula dhalimu wa Uhuru,” Kuria aliandika.

Mbunge huyo wa Gatundu ya Kusini pia alisema kwamba Wamae anajua vizuri sana kiasi cha takrima ambayo Wajackoyah anapokezwa kutoka ikulu kupitia mchanganuzi wa kisiasa Mutahi Ngunyi, kiasi ambacho Kuria anadai Wamae amekuwa akilalama kwamba hakimfikii yeye kama mgombea mwenza wa Wajackoyah.

“Unajua Wajackoyah anapokea pesa ngapi kutoka kwa Jimbo kupitia Mutahi Ngunyi. Unajua umekuwa ukimlalamikia Chini ya maji kuwa hashiriki nyara na wewe,” Kuria alidai.

Kwa maana hiyo, Kuria alinrai Wamae kujifanyia heshima japo kiasi tu kwa kujiondoa katika nafasi hiyo ya kuwa mgombea mwenza wa Wajackoyah, huku akimuahidi kwamba yeye kama ndugu yake atakuwa nyuma yake katika maamuzi hayo.

“Sasa rafiki yangu Wangui kuwa na ujasiri kiasi na uache tikiti hiyo. Kama kaka yako nipo nyuma yako kwa hili,” Kuria alimshauri Wamae.