(Video) "Atwoli hashughulikii mtoto, Ruto nisaidie mtoto asome" Mkewe Francis Atwoli aomba msaada

Alisema mtoto tangu mwaka uanze hajaenda shule juu ya karo.

Muhtasari

"Kuna mtu mmoja ambaye ameacha bibi hata na mtoto" - Roselinder alisema.

Roselinder Simiyu, mke mtalikiwa wa katibu mkuu wa muungano wa wafanyakazi nchini COTU, Francis Atwoli kwa mara nyingine tena amezua gumzo mitandaoni baada ya kudai kwamba Atwoli tangu amwache hajawahi shughulikia mtoto karo na kumtaka naibu wa rais William Ruto kuingilia kati na kumsaidia.

Katika video ambayo imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Rosilinder Simiyu anaonekana akimsihi Ruto kumsaidia kulipia mtoto karo huku akisema kwamba Atwoli amekuwa gumegume ambaye hajawahi mshughulikia mtoto kwa zaidi ya mwakqa mmoja sasa.

“Unahukumiwa kulingana na kundi unajiweka. Kuna mtu mmoja ambaye ameacha bibi hata na mtoto. Mheshimiwa Ruto naomba, niko na mtoto ambaye tangu mwaka uanze hajaenda shuleni, najua Atwoli amekutukana, lakini kwa niaba ya mama, nisaidie mtoto aende shuleni,” alisema Roselinder kwenye video hiyo.

Mapema mwaka huu ,Roselinder alitingiza tasnia ya siasa nchini baada ya kutangaza kumuunga mkono naibu rais William Ruto katika kinyang’anyiro cha urais, huku akiendqa kinyume na aliyekuwa mumewe, Francis Atwoli ambaye kwa muda mrefu amekuwa akimtemea Ruto cheche kali akisema kwamba hata kwa dawa naibu rais hawezi kuwa mrithi wa rais Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 9. Atwoli anampigia debe kinara wa Azimio-One Kenya, Raila Odinga.

Roselinder Simiyu anawania uwakilishi wa kike katika kaunti ya Bungoma na alitumia fursa hiyo kujipigia debe huku akisema kwamab yeye anajua maumivu kama mama ambaye ameachwa na mtoto bila kushughulikiwa mahitaji ya shuleni na kusema kwamba pindi atakapochaguliwa watu wakienda kwake kwa matatizo ataelewa na kutoa usaidizi.

“Na mimi nawaomba mimi najua, kama mama ambaye amekosa karo ya shule, ninaomba mnipe kura, mkinipa hiyo kura, ukija kwangu wakati unahitaji usaidizi, nitaelewa na nitakusaidia, Mungu awabariki,” alimaliza kuhutubu.

Tamko hilo lake kwamba Atwoli hashughulikii mtoto limepata mpenyo mkubwa kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi wakidai suaal hilo si kweli na kusema ni kama njia moja ya kumchafulia katibu huyo wa COTU jina haswa msimu huu wa siasa ambapo propaganda zinatumika kueneza sera dhidi ya wapinzani, huku wengine wakimsuta Atwoli kwa kujidai kupasua simu zenye gharama kubwa kwenye mahojiano mubashara ya runinga hali ya kuwa mtoto wake anaungulia machungu ya kukosa elimu.