Uhuru Kenyatta: Martha Karua hatacheka na waporaji

Rais Kenyatta alisema Martha Karua hatongoja kuwafunga wafisadi pindi Azimio itakapochukua uongozi wa nchi hii.

Muhtasari

• Rais pia alimsuta naibu wake kwamba badala asaidie, anazunguka akijipiga debe na mazuri ya Jubilee huku akiyakana mabaya.

Mgombea mwenza wa Azimio Martha Karua na rais Uhuru Kenyatta
Mgombea mwenza wa Azimio Martha Karua na rais Uhuru Kenyatta
Image: Facebook

Sasa ni wazi na rasmi kwamba rais Uhuru Kenyatta kwa mara nyingine baada ya kimya kirefu amejitosa kwenye dimbwi la siasa huku safari hii akiwa muwazi zaidi katika kunadi sera za Raila Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua kwa wananchi.

Jana alipozuru eneo bunge la Kasarani kuzindua hospitali moja eneo hilo, rais Kenyatta kwa ukakamavu alimpigia debe Raila Odinga na kumtaja kuwa mtu pekee ambaye ataleta amani na maendeleo katika taifa la Kenya pindi atakapochaguliwa kama rais wa kumrithi yeye.

Aidha, rais pia hakusita kumsifia mgombea mwenza wa Raila Odinga, mama Martha Karua huku akimtaja kuwa mama ambaye hacheki na wafisadi na kuwahakikishia wananchi kwamba Karua atachapa kazi na kuwafunga jela waporaji wa mali ya umma, na wala hatalegeza kama kama ambavyo yeye alivyofanya kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita wakati wa utawala wake kama rais wa nne.

“Mama ambaye hacheki, Martha Karua, na ambaye hatangojea kusikia mambo ya hawa waporaji wakifanya mambo yao huku na huku,” rais alisema.

Pia alimrushia bomu la moto naibu wake William Ruto huku akisema hakuna vile anaweza jitenga na mabaya ya chama cha Jubilee huku akijihusisha na kujijipia debe na mafanikio ya serikali hiyo kwa wakati mmoja.

“Badala akuje kutusaidia, kazi yake ni kupiga mdomo na yeye mwenyewe ako ndani ya serikali. Anajaribu kusema ukiona barabara ni yeye, ukiona njaa ni mwingine, kwani serikali ni mbili?” rais alisema.

Rais Kenyatta alimtaka naibu wake kunadi sera zake kwa njia inayofaa na si kutumia uongo ili kuwatupia wakenya changa la macho kwa sababu ya kutaka kura kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.