Wamalwa: Ruto mimi nakuheshimu, hujafanya vizuri kunitukana mwanamke

Wamalwa alisisitiza kwamba alichokisema ni ukweli kwamba nusra yeye na mwenzake Dkt. Matiang'i wazabwe kofi na Ruto mwaka 2018.

Muhtasari

• Waziri huyo wa ulinzi ndiye alianza chokoza chokoza kwa kusema kwamba nusra naibu rais amzabe kofi mwaka 2018.

• Jana Ruto alimjibu kwa kejeli huku akisema kwamba kwa mila zao huwa hawapigi wanawake makofi.

• Wamalwa amekosoa maneno hayo ya Ruto akisema ni kama kumshushia heshima kwa kumuita mwanamke.

Waziri wa ulinzi Eugene Wamalwa na naibu rais William Ruto
Waziri wa ulinzi Eugene Wamalwa na naibu rais William Ruto
Image: Twitter

Waziri wa ulinzi Eugene Wamalwa amemjibu naibu rais Kenyatta kuhusu madai yake ya kumuita mwanamke wakati alikuwa anajibu shtuma kwamba alijaribu kuwazaba makofi na kumfuta kazi mwaka 2018.

“Amenitusi sana. Ruto nataka nikuambie kwa heshima sana, nakuheshimu, mimi sijawahi kutusi, nakuheshimu sana. Chenye ulisema leo na matusi kwa Eugene Wamalwa ni maneno kabisa ambayo hayaoneshi wewe kuwa mtu anayetaka kuwa rais kabisa. Nikisema ukweli ya kwamba William Ruto ulitaka kunipiga kofi 2018, ni ukweli,” alilalama Wamalwa.

Jana katika hafla ya kisiasa Magharibi mwa Kenya, mgombea urais kupitia tikiti ya chama cha UDA na muungano wa Kenya Kwanza Dkt. William Ruto alijibu madai ya Wamalwa aliyoyatoa wikendi iliyopita kwamba Ruto nusra amzabe kofi mwaka wa 2018.

Wikendi ilizopita, Waziri Wamalwa aliibua madai kwamba William Ruto alikuwa nusra kumzaba kofi yeye na mwenzake wa usalama wa ndani Dkt. Fred Matiang’i baada ya wawili hao kuandaa mkutano wa viongozi kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya pasi na kumshirikisha.

Wamalwa alisema kinyume na rais ambaye alisema kwamab iwapo Ruto angemzaba kama ambavyo mkanda wa sauti uliosambazwa ulikuwa unasema basi yeye angemgeuzia upande wa shavu la pili, Wamalwa alisema yeye angemjibu Ruto kwa ngumi kali kama ya mwanamasumbwi mkonge wa Kimarekani, Mike Tyson.

“Tulikuwa na mkutano na rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi ambapo tulikuwa na ndugu zangu kutoka NASA, Musalia Mudavadi, Wetangula, Oparanya na wengine, naibu raisc alikasirika vikali kuhusu ni kwa nini nilichukuwa viongozi wa Abaluhya kwenye ikulu bila kumjulisha, aliniambia niondoke ofisini mwake na nipeleke barua ya kuacha kazi. Karibu nipate kofi ya huyo jamaa. Lakini angeteleza iniguse ningempa uppercut moja,” Wamalwa alijigamba katika mkutano moja wa Azimio-One Kenya.

Naibu rais sasa ameonekana kumjibu Waziri huyo anayeegemea upande wa rais Kenyatta na Raial Odinga huku akimuambia kwamba katika mila zao, huwa hawapigi kofi wanawake – kwa maana nyingine naibu rais amemtaja Waziri Wamalwa kama mwanamke.

“Nilisikia jamaa mwingine ambaye nilimpatia kazi ya Waziri ati anasema mimi nilikuwa nataka kumpiga makofi. Mimi nataka nimuambie huyu jamaa, unajua huko kwetu hatuchapi kofi wanawake, eeh mmuambie hivo na mwambie awache mdomo mrefu. Bila mimi angekuwa anatembea barabarani. Mimi ndio nimemtoa kwa mtaro nikampatia kazi ya Waziri,” Ruto alimtupia bomu la moto Wamalwa.